May 09, 2016 07:03 UTC
  • Yanga Hoyee
    Yanga Hoyee

Yanga yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania; Leicerster watuzwa rasmi Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza; Orodha mpya FIFA, nchi yako iko katika nafasi ya ngapi? Mchezaji wa Cameroon aanguka ghafla uwanjani na kuaga dunia papo hapo.

Muirani ashinda dhahabu Fajr Open Taekwondo

Bingwa wa mchezo wa taekwondo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Kazemi ametia kibindoni nishani ya dhahabu katika duru ya 27 ya Mashindano ya Fajr Open jijini Tehran. Siku ya Jumamosi, Kazemi alishiriki fainali katika kitengo cha wanaume wenye uzani usiozidi kilo 58 na kumbwaga Vahid Alemi wa Afghanistan kwa alama 3-1 na kutwaa medali ya dhahabu. Yousif Ben Shariha kutoka Libya na Muirani Hadi Tiranvalipour kwa pamoja walishinda medali ya shaba. Katika kitengo cha wenye uzani usiozidi kilo 80, raia wa Russia Arutiun Meliksetiants alimlemea Muirani Amir Hossein Sasan katika pigano la finali na kumzaba kwa alama 14-10 na kutwaa dhahabu. Wairani Vahid Isabiglo na Pourian Erfanian kwa pamoja waliondoka na medali ya shaba. Duru ya 27 ya Fajr Open Taekwondo ilifanyika kati ya Mei 7 na 8 hapa Tehran kwa kuwashirikisha wanataenwondo kutoka Iran, Afghanistan, Azerbaijan, Brazil, India, Armenia, Iraq, Libya, Russia na Uturuki.

Shirikisho la Soka Iran lapata rais mpya

Mehdi Taj amechaguliwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la Soka la Iran IFF. Katika uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa olimpiki jijini hapa siku ya Jumamosi, Taj alijinyakuliwa kura 50 akifuatiwa na Mostafa Ajoulou aliyepata kura 15. Aziz Mohammadi aliibuka katika nafasi ya tatu kwa kujizolea kura 6. Mehdi Taj anatazamiwa kuliongoza shirikisho hilo kwa muda wa miaka minne, yaani hadi mwaka 2020. Taj ambaye alikuwa naibu rais wa Shirikisho la Soka la Iran amekuja kurithi mikoba ya Ali Kaffashian ambaye ameongoza taasisi hiyo ya mpira wa miguu nchini kwa kipindi kirefu zaidi katika historia ya shirikisho hilo, yaani miaka minane na miezi minne.

Orodha ya FIFA, Uganda yaongoza Afrika Mashariki, Argentina duniani

Timu ya taifa ya soka ya Uganda maarufu The Cranes imeendelea kusalia kileleni mwa orodha ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA katika kanda ya Afrika Mashariki. Taifa Stars ya Tanzania imeorodheshwa ya mwisho Afrika Mashariki katika orodha mpya ya FIFA na nafasi ya 129 duniani. Mbali na kuongoza Afrika Mashariki, Uganda imejizatiti na kukwea hadi katika nafasi ya 72 duniani, huku Rwanda katika nafasi ya 87. Kenya ambayo viwango vyake vya soka vimekuwa vikififia kila uchao ipo katika nafasi ya 116 huku Burundi ikitosheka na nafasi ya 122. Kwa ujumla Argentina bado inaendelea kuongoza katika orodha hiyo ikifuatiwa na Ubelgiji huku Chile ikifunga orodha ya tatu bora. Mabingwa wa kombe la dunia Ujerumani wanashikilia nafasi ya nne huku Uhispania na Brazil zikifuata katika nafasi ya tano na sita kwa usanjari huo. Timu ya bara la Afrika inayochukua nafasi nzuri kwenye orodha hiyo ya FIFA ni Algeria iliyopo katika nafasi ya 33 ikifuatiwa na Ivory Coast katika nafasi ya 34.

Yanga yatwaa taji la Ligi Kuu ya Soka Tanzania

Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka nchini humo na sasa inasubiri tu kukabidhiwa taji hilo rasmi. Baada ya klabu hiyo kuhitaji pointi tatu ili itangazwe kuwa bingwa wa ligi, mchuano wa Jumapili kati ya Simba na Mwadui FC uliipa ubingwa Yanga kwa kuwa Simba ndio ilikuwa kwenye mbio za kuwania ubingwa sambamba na Yanga. Shamrashamra za mashabiki wa Yanga zilianza Jumapili nje ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, licha ya klabu hiyo kutocheza siku hiyo baada kucheza Jumamosi dhidi ya Eseperance ya Angola. Klabu hiyo iliichabanga timu hiyo ya Angola mabao 2-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho. Goli la dakika ya 73 la Mwadui FC lililofungwa na Jamal Mnyate liliifanya Simba kukosa matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania, hata kama watashinda mechi zao tatu zilizobakia na Yanga wakafungwa mechi zote tatu.

Yanga hadi sasa wana point 68 wakati Simba wana point 58 hivyo wakishinda mechi zao tatu watakuwa na point 67, pointi moja nyumba ya Yanga.

Hatimaye Leicerster yatwaa Ligi ya Premier

Hatimaye klabu ya soka ya Leicerster City imetuzwa kombe lake la kwanza la Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuibuka kidedea msimu huu na kumaliza ikiwa na pointi 80. Hafla za kuwatuza wanasoka hao zilifanyika Jumamosi nyumbani katika uga wa King Power, baada ya kuitandika Everton mabao 3-1 mbele ya mashabiki zaidi ya 32 elfu. Hata hivyo kutwaa kombe hilo hakukutegemea zaidi ushindi wao dhidi ya Everton katika kipute hicho cha mwisho, bali sare ya mabao 2-2 katika mechi kati ya Chelsea na Tottenham Hotspurs wiki iliyopita ndiyo iliyowahakikishia ubingwa vijana wa The Foxes.

Katika mchuano huo wa mwisho Jumamosi, Leicester City waliwaadhibu wageni wao Everton mabao 3-1 na kuupa maana msemo unaosema 'mcheza kwao hutuzwa.' Jamie Vardy aliifungia klabu hiyo mabao mawili, la kwanza kunako dakika ya 5 na la pili katika dakika ya 65 kupitia mkwaju wa penati. Andy King alicheka na nyavu dakika ya 33 ya mchezo na kuwahakikishia Foxes ushindi laini wa nyumbani. Goli la kufuia machozi la Everton lilifungwa na Kevin Mirallas dakika ya 88.

Hili ndilo Kombe la kwanza la Ligi ya Premier kutwaliwa na klabu ya Leicester City iliyoanzishwa miaka 132 iliyopita, na pia taji la kwanza la Ligi Kuu kwa kocha wao Claudio Ranieri ambaye amewahi kuvifundisha vilabu ya Napoli, Inter Milan, Chelsea, Atletico Madrid na Juventus bila kutwaa taji hilo. Mfanyabiashara bilionea wa Thailand, Vichai Srivaddhanaprabha ambaye ni mmiliki na mwenyekiti wa timu hiyo ametangaza kutoa zawadi mbalimbali kwa wachezaji wa kikosi cha Leicester msimu huu kutokana na mafanikio yao. Kwa kuanzia kila mchezaji atapewa gari aina ya Mercedes B-Class Electric Drive yenye thamani ya pauni 32,670, na hii inamaanisha kuwa bilionea huyo atalazimika kujikamua kiasi cha dola milioni 1 za Marekani kutimiza ahadi hiyo. Na kama hilo haitoshi, tajiri huyo tayari ameshatoa ahadi kwa kikosi cha Claudio Ranieri kwenda kujivinjari katika jiji la anasa la Las Vegas kwa gharama zake katika kipindi cha likizo. Pia bilionea huyo atawapa kiasi cha pauni 6.5 milioni ambazo watagawana kama makubaliano ya bonasi zao endapo wangetwaa ubingwa. Kinachosubiriwa kwa sasa kwenye Ligi ya Premier ni kuona ni nani atakayeibuka katika nafasi ya pili, ya tatu na ya nne wakati ambapo wachambuzi wengi wa soka wametoa bishara kuwa Man U itamaliza katika nafasi ya tano.

Ligi ya Uropa: Fainali Liverpool na Sevilla

Klabu ya Liverpool inatazamiwa kushuka dimbani kumenyena na Sevilla katika mchuano wa finali ya Ligi ya Uropa (Europa League). Baada ya kutandikwa bao 1-0 na Villareal kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uhispania, mchuano wa marudio usiku wa Alkhamisi mambo yalikuwa tofauti. Liverpool ikiwa nyumbani Anfield ilishusha kipigo cha maana kwa Villarreal cha mabao 3-0 na kutinga fainali ya Europa League itakayopigwa baadaye mwezi huu mjini Basel, Uswisi. Liverpool ilihitaji dakika saba tu kupata bao la kuongoza baada ya Bruno Soriano kujifunga kabla ya kufunga mengine mawili katika kipindi cha pili kupitia kwa Daniel Sturridge na Adam Lallana na hivyo kukata tiketi ya fainali ambapo watakwenda kumenyana na Sevilla ambao walitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Shakhtar Donetsk jumla ya mabao 5-3 baada ya ushindi wao wa 3-1 usiku wa Jumatano. Fainali hiyo ya kukata na shoka itapigwa Mei 18 katika dimba la St. Jakob-Park mjini Basel, nchini Uswisi. Sevilla walilibeba taji hilo kwa misimu miwili mfululizo, mwaka 2014 na mwaka 2015, hivyo wamerudi tena fainali kutetea ubingwa wao. Liverpool sasa wamejiweka kwenye nafasi tamu ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kama watabeba taji hilo la Europa League hata kama kwenye Ligi Kuu ya Uingereza watamaliza nje ya nne bora. Kwa sasa kikosi hicho kinachonolewa na Jurgen Klopp kinashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.

Dondoo: Tanzia

Ulimwengu wa soka unaendelea kuomboleza kifo cha ghafla cha kiungo wa klabu ya Dinamo ya Romania kilichotokea uwanjani Ijumaa iliyopita. Mchezaji huyo wa soka ya kulipwa Patrick Ekeng raia wa Cameroon alianguka uwanjani bila kuguswa na yeyote na kukafariki dunia papo hapo. Ekeng, mwenye umri wa miaka 26, alianguka na kuaga dunia papo hapo kunako dakika ya 70, ikiwa ni baada yake kucheza kwa muda wa dakika saba pekee. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa ameingizwa kama nguvu mpya kwenye mchuano dhidi ya Viitorul. Hii si mara ya kwanza kwa mchezaji wa Cameroon kufariki akiwa uwanjani. Mnamo Juni 26 mwaka 2003, kiungo Marc-Vivien Foe alianguka ghafla dakika ya 73 na muda mchache baadaye akafariki wakati Cameroon ilikuwa ikicheza dhidi ya Colombia kwenye Kombe la Mashirikisho, hatua ya nusu-fainali katika uwanja wa Lyon's Stade de Gerland.


......................................................TAMATI......................................................


Tags