Apr 10, 2021 02:29 UTC
  • Jumamosi, 10 Aprili, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Shaaban 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 Miladia huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25. ***

Joseph-Louis Lagrange

 

Miaka 176 iliyopita katika siku kama ya leo aliuawa Sayyid Ali Muhammad Shirazi aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya “Bab” ambaye alidai kuwa ndiye Imam Mahdi (AF) na baadaye akadai kuwa ni Mtume. Alizaliwa mwaka 1235 Hijria Qamariya katika mji wa Shiraz nchini Iran na alionekana kuwa na itikadi potofu akiwa bado shuleni. Muhammad Ali Bab ambaye hakuwa na elimu ya juu alifuatwa na watu majahili na kuungwa mkono na wakoloni. Baada ya kudai kuwa ndiye Imam wa mwisho katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) yaani Imam Mahdi (AF), Bab alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba dini ya Uislamu imefutwa. Wanazuoni wa zama hizo walifichua urongo wake na kuchukulia hatua. Hata hivyo aliendelea kulingania itikadi zake potofu na katika siku kama ya leo Amir Kabiir aliyekuwa kiongozi wa zama za Qajar alitoa amri ya kunyongwa kwake. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 Miladia sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa. ***

Emiliano Zapata

 

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon. Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946. ***

Bendera ya Lebanon

 

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO). Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina. ***

 

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita inayosadifiana na 21 Farvardin 1367 Hijria Shamsia, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia mji wa Marivan wa magharibi mwa Iran na kukilenga kijiji kimoja kwa mabomu ya kemikali. Raia kadhaa waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika jinai hiyo ya utawala wa Saddam Hussein. Jamii ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi zilinyamazia kimya jinai hiyo na badala yake zilitoa misaada zaidi ya silaha za kemikali kwa nchi hiyo. ***

Wahanga wa mashambulio ya kemikali dhidi ya mji wa Marivan wangali wanataabika

 

Na katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Farvardin 1378 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Meja Jenerali Ali Sayyad Shirazi, Kaimu Kamanda Mkuu wa majeshi yote na mmoja kati ya makamanda shupavu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kufyatuliwa risasi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin mjini Tehran. Meja Jenerali Shirazi alikuwa mwanaharakati wa mapinduzi, na alitupwa gerezani mara kadhaa wakati wa utawala wa Shah, na hatimaye aliachiliwa huru baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Meja Jenerali Sayyad Shirazi aliwahi kuwa Kamanda wa Jeshi la nchi kavu wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. ***

Ali Sayyad Shirazi

 

Tags