Apr 18, 2021 06:12 UTC
  •    Jumapili, Aprili 18, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 5 Ramadhani 1442 Hijria Qamaria sawa 29 Farvardin 1400 Hijria Shamsiya ambazo ni sawa na Aprili 18 2021

Siku kama ya leo miaka 796 iliyopita, yaani tarehe 5 Ramadhani mwaka 646 Hijria Qamaria, alifariki dunia Afdhaluddin Abu Abdillah Khunji, mtoto wa kiume wa Abdul Malik Khunji, katika karne ya 7 Hijria Qamaria. Alizaliwa mwaka 590 Hijria Qamaria katika mji wa Khunji katikati mwa mkoa wa Khalkhal, kaskazini magharibi mwa Iran, ambako alijifunza elimu ya msingi. Msomi huyo wa Kiislamu ambaye alikuwa mtu mwenye hekima na busara, alikuwa mhadhiri wa masomo ya tiba na pia masomo ya Kiislamu kama Fiqhi na Hadithi. Miongoni mwa kazi zake ni kitabu kiitwacho "Kashful Asrar an Qhawamidhul Afkaar Fii Mantiq".

Katika siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, inayosadifiana na Ramadhani 5 mwaka 1236 Hijria, al-Haji Mulla Ali Aliyari Tabrizi mmoja wa maulama mahiri wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Alitabahari katika elimu za fikihi, hadithi, mashairi na fasihi kama ambavyo alikuwa mahiri pia katika elimu za nujumu na hisabati. Al-Haji Mulla Ali Aliyari Tabrizi aliwahi kufanya safari na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Najaf Iraq ambapo akiwa huko alifanikiwa kunufaika na elimu za wanazuoni mahiri katika zama hizo kama Sheikh Murtadha Ansari na Mirza Shirazi na hivyo kuwa na umahiri mkubwa katika Fikihi na Usuul al-Fikih. Mwanazuoni huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi vyenye thamani kubwa. Moja ya vitabu vyake ni "Dalailul Ahkaam fii Sharh Sharai'i al-Islam." 

Mulla Ali Aliyari Tabrizi

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran.  Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa mwana wa marhoum Hujjatul Islam wal Muslimin Hajj Sayyid Javad Husseini Khamenei na alikuwa mtoto wa pili katika familia. Maisha ya Sayyid Javad Khamanei, sawa na ya wanazuoni wengi yalikuwa sahali na ya kawaida kabisa. Ayatullah Khamenei alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza masomo  chini ya usimamizi wa mwanazuoni na marjaa maarufu Ayatullahil Udhma Milani. Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na kisha baada ya hapo, aliwahi pia kuchaguliwa kuwa mbunge na pia mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Aidha alikuwa Rais wa Iran katika duru mbili mfululizo na hatimaya mwaka 1989, baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi wa pili wa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdel Nasser alifanya mapinduzi dhidi ya Muhammad Nagib na kuwa Rais wa nchi hiyo. Gamal Abdel Nasser ndiye aliyetaifisha na kuitangaza kuwa mali ya taifa Kanali ya Suez na alikuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na ubeberu katika ulimwengu wa Kiarabu na barani Afrika. Aidha rais huyo wa zamani wa Misri alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. 

Gamal Abdel Nasser

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, mkutano wa kwanza wa wawakilishi wa nchi za Asia na Afrika uliojulikana kwa jina la Mkutano wa Bandung ulifanyika katika mji wenye jina hilo nchini Indonesia. Mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 29 za Asia na Afrika, ulikuwa na lengo la kujenga umoja wa nchi hizo za ulimwengu wa tatu katika kukabiliana na kambi kubwa mbili duniani za Mashariki na Magharibi. Mkutano wa Bandung ndio ulioandaa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM)

Mkutano wa Bandung

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Aprili 1980, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilipata uhuru. Zimbabwe ilikoloniwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19. Mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kufuatia kudhoofika Uingereza, zilianza harakati za wananchi za kupigania uhuru na hatimaye harakati hizo zilipelekea kuundwa makundi ya mapambano ya silaha. Zimbabwe ina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 390,000 na inapakana na nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Afrika Kusini. 

Bendera ya Zimbabwe

 

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 18 Aprili 1996, jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia makao ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon. Katika shambulizi hilo la kinyama la Wazayuni, takribani raia 110 wa Lebanon waliuawa shahidi wakiwemo wanawake na watoto. Licha ya hayo, Marekani ilizuia kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio la kulaani mauaji ya kijiji cha Qana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Mauaji ya Qana

Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 29 Farvardin mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  lilitangaza utiifu kwa Imam Khomeini (MA) Hayati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Siku hiyo Jeshi lilitangaza utiifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mnasaba huo likaandaa gwaride zisizo na kifani kote Iran.

Gwaride hizo zilipokelewa kwa vuraha na wananchi Waislamu wa Iran kwani zilikuwa ni dhihirisho la mshikamano wa wananchi na jeshi katika njia ya kulinda Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Kiislamu. Kwa msingi huyo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku hiyo hutambuliwa kama 'Siku ya Jeshi' na kila mwaka huandaliwa gwaride maalumu kwa mnasaba huo.

Gwaride la Jeshi la Iran