May 10, 2021 22:22 UTC
  • Jumanne tarehe 11 Mei mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe 28 Ramadhani 1442 Hijria sawa na Mei 11 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1170 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake, Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Mad'khal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.

Tarehe kama ya leo miaka 157 iliyopita alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21 Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960.

Ethel Lilian Voynich

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho cha kwanza cha matangazo ya televisheni kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa  wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha.

Paul Gottlieb Nipkow

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya pamoja ya Ufaransa na Uingereza yaliwasili nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. Hatua hiyo ya Ufaransa na Uingereza ya kuiunga mkono Ubelgiji ilikuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwako baina ya nchi hizo. Licha ya kuweko muungano huo wa kijeshi, vikosi vya Ujerumani ya Kinazi mbali na kuyashinda majeshi ya Ubelgiji vilivishinda pia vikosi vya  pamoja vya Uingereza na Ufaransa na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi hiyo.

Vita vya Kwanza vya Dunia