May 15, 2021 00:00 UTC
  • Jumamosi, 15 Mei, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 3 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na tarehe 15 Mei, 2021 Miladia.

Tarehe 25 Ordibehesht ni siku ya kumbukumbu ya Abul-Qassim Firdowsi mwanafalsafa na malenga mashuhuri wa Iran. Inasemekana kuwa Firdowsi alizaliwa mwaka 319 au 320 Hijria Shamsia katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh". Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa kwa lugha mbali mbali. ***

 

Abul-Qassim Firdowsi

 

Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1776 Miladia, ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini. ***

Meli inayotumia mvuke

 

Miaka 162 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1859 Miladia, alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906. ***

Pierre Curie na Marie Pierre

 

Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1862 Miladia, alizaliwa Arthur Schnitzler mwandishi wa visa wa nchini Austria. Bibi na babu wa Arthur walikuwa matabibu na kutokana na hali hiyo, yeye pia akasomea taaluma hiyo na kufanikiwa kupata shahada katika uga huo. Hata hivyo aliachana na taaluma hiyo na kujiunga na taaluma nyingine aliyokuwa akiipendelea, yaani ya uandishi. Arthur Schnitzler pia alikuwa na ujuzi katika masuala ya kisaikolojia ambapo aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Kasuku wa Kijani' 'Ardhi Pana' na 'Kuruka Kuelekea Kwenye Giza.' Arthur Schnitzler alifariki dunia mwaka 1931 Miladia. ***

Arthur Schnitzler

 

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Izmir iko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianzia katika mji huo wa kihistoria. ***

Izmir Uturuki

 

Katika siku kama ya leo 81 iliyopita,  jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tangu tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru wake mwaka 1945. ***

Kukaliwa kwa mabavu Uholanzi na Ujerumani ya Kinazi

 

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Mei 15 kuwa Siku ya Kimataifa ya Familia. Uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na umuhimu wa familia na asasi hii tukufu ambayo inahesabiwa kuwa msingi mkuu wa jamii na lengo ni kuilinda familia na madhara ya nje na ya ndani na kuifanya iwe na mchango na nafasi bora zaidi. Asasi ya familia ilikuweko tangu wakati wa kudhihiri mwanadamu na imeendelea kuwa nguzo kuu ya jamii.  Mke na mume na watoto na wakati mwingine bibi na babu ni watu wanaounda familia hii. Familia ni mahala tulivu kwa wenza, sehemu ya kulea na kukuza watoto na ni mazingira yenye amani kwa ajili ya wanafamilia kuwa na mawasiliano salama.***

Siku ya Kimataifa ya Familia