Jumatatu tarehe 17 Mei mwaka 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 5 Shawwal 1442 Hijria sawa na 17 Mei mwaka 2021
Katika siku kama ya leo tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 60 Hijria Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein (as) aliwasili katika mji wa Kufa, moja ya miji ya Iraq, kwa shabaha ya kuwalingania wenyeji wa eneo hilo kwenye njia ya kweli na haki. Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua kadhaa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) wakimuomba aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidikteta wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim Bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein (as) iliyowalingania kujiunga na harakati ya kiongozi huyo. Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein, lakini baadaye walikengeuka. Mwishowe watu wa Kufa walimuacha peke yake Muslim Bin Aqil, na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari wa utawala wa Bani Umayyah.

Miaka 272 iliyopita, katika siku kama hii ya leo alizaliwa Edward Jenner, tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui tarehe 14 Mei mwaka 1796 akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Baada ya hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Maradhi hayo ambayo wakati huo yalikuwa yakichukua roho za watu bila ya huruma, yalitokomezwa kabisa duniani mwaka 1979.
Miaka 156 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa. Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano. Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya. Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa.

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kilichopewa jina la "Kitabu Cheupe" (The White Paper) na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa vita vya kulazimishwa vya majeshi ya Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndege za kivita za Iraq ziliishambulia manowari ya kivita ya Marekani iitwayo Stark katika eneo la Ghuba ya Uajemi, na kupelekea wanajeshi 37 wa Kimarekani kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Baada ya tukio hilo, utawala wa Saddam uliomba radhi kwa serikali ya Marekani na kutangaza kuwa tayari kulipa fidia za uharibifu huo.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.