Jumamosi, Mei 22, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 22 Mei 2021 Miladia.
Tarehe Mosi Khordad mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ni siku ya kumuenzi Muḥammad Saddruddin Qawam Shirazi maarufu kama Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa. Alizaliwa tarehe 9 Jamadil Ula mwaka 980 Hijria Qamaria mjini Shiraz. Awali alielekea katika mji wa Qazvin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Amma elimu nyingine kuhusu maumbile, hisabati, nujumi na nyota alitabahari nazo kupitia kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake. Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 huku kitabu cha Hikmat Al Muta'alyahfi-l-asfar al-‘aqliyya al-arba‘a kikiwa maarufu zaidi kuliko vitabu vyake vingine. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria mjini Basra, Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na akazikwa katika mji huo huo. ***
Siku kama ya leo miaka 1114 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Muqlah, mwandishi, mwanakaligrafia na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji. Alizaliwa Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo. Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Bani Abbas akiwa kijana. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala wake, msomi huyo alikamatwa na kufungwa jela. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi. Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalatun fi Mizaanil-Khat.'***

Miaka 136 iliyopita, katika siku kama hii ya leo sawa na tarehe 22 mwezi Mei mwaka 1885 aliaga dunia mwandishi na malenga mtajika wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83 kwa jina la Victor Hugo. Hugo alikuwa mfuasi wa mageuzi kwa maslahi ya wale waliokandamizwa na kudhulumiwa. Alizaliwa mwaka 1802 miladia na alianza kughani mashairi tangu akiwa kijana. Akiwa na umri usiopindukia miaka 25 Hugo alikuwa mwanachama katika akademia ya Ufaransa na wakati huo huo akawa mbunge katika bunge la Ufaransa. Victor Hugo aliamua kuachana na masuala ya siasa wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu kutokana na kupinga kwake siasa za kibeberu za mtawala huyo na kuelekea uhamishoni kwa miaka 20. ***
Miaka 41 iliyopita tarehe Mosi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianza. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran kwa lengo la kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran. Aidha lengo la mzingiro huo wa kiuchumi lilikuwa ni kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ukubali kuwa na uhusiano wa kawaida na Marekani. Kufuatia uamuzi huo wa utawala wa Marekani, Imam Khomeini MA, muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alitangaza bayana kuwa uhai wa kiuchumi wa mataifa hautegemei madola makubwa na akilihutubu taifa la Iran alisema: "Msitishwe hata kidogo na mashinikizo hayo ya kiuchumi kwani iwapo watatuwekea vikwazo vya kiuchumi watakuwa wametupa fursa ya sisi wenyewe kujitegemea kiuchumi. Watu wanaotishwa na vikwazo vya kiuchumi ni wale wanaoona kuwa uchumi ndio msingi wa kila kitu na dunia ndio mwanzo na mwisho wao."***
Na siku kama hii ya leo miaka 35 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Mwaka 1924. Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo. ***