May 22, 2021 22:17 UTC
  • Jumapili tarehe 23 Mei mwaka 2021

Leo ni Jumapili tarehe 11 Shawwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Mei mwaka 2021

Tarehe 11 Shawwal miaka 1439 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu.

Katika siku kama ya leo miaka 403 iliyopita, sawa na 23 Mei 1618, kulianza vita vya kidini barani Ulaya vilivyoendelea kwa muda wa miaka 30. Katika vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark zilikuwa zikiwaunga mkono Waprotestanti, huku Uhispania na Ufalme wa Rome zikiwaunga mkono Wakatoliki. Vita hivyo vilifikia tamati mwaka 1648 baada ya kutiwa saini Mkataba wa Westaphalia.

Vita vya kidini vya miaka 30 barani Ulaya

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 na shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu. 

Henrik Ibsen

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Othmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi. Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo. 

Vita vya Kwanza vya Dunia

Na katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, alijiua Heinrich Himmler Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi na Usalama la Ujerumani ya Kinazi. Himmler alizaliwa mwaka 1900 na alipofikisha umri wa miaka 34 aliweza kupanda cheo na kuwa mkuu wa shirika hilo la kijasusi na usalama la Ujerumani (Gestapo). Heinrich Himmler anahesabiwa kuwa mmoja kati ya viongozi wauaji na wamwagaji damu ambaye aliongoza operesheni kadhaa za mateso na kuuwa watu nchini humo. Himmler alitiwa mbaroni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya Nurenberg nchini Ujerumani, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo aliamua kujiua mwenyewe baada ya kunywa sumu.

Heinrich Himmler