Jumapili tarehe 30 Mei 2021
Leo ni Jumapili tarehe 18 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na Mei 30 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 243 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 188 iliyopita Mirza Hussein Nuri, alimu na faqihi mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Nur kaskazini mwa Iran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, Mirza Hussein Nuri alielekeza juhudi na jitihada zake katika masuala ya kujifunza na kukusanya Hadithi. Msomi huyo wa Kiislamu alitokea kuwa mmoja wa wanazuoni wakubwa wa masuala ya Hadithi na baadaye akaanza kuandika vitabu vya thamani katika uwanja huo. Miongoni wma vitabu hivyo ni Akhbaru Hifdhil Qur'an, Risala ya Tuba na Muhtasari wa Historia ya Viongozi wa Uislamu.

Siku kama ya leo 97 miaka iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atibaa, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alianza kujifunza masomo ya kidini na udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atibaa katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada kubwa katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.'

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Ziaur Rahman, Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Ziaur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo.