May 31, 2021 22:12 UTC
  • Jumanne tarehe Mosi Juni mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe 20 Shawwal 1442 Hijria sawa na tarehe Mosi Juni mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 625 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".

 

Miaka 98 iliyopita muwafaka na siku kama ya leo, moja kati ya zilzala kubwa zilizouwa watu wengi duniani, iliikumba Tokyo mji mkuu wa Japan. Zilzala hiyo ilitokea nyakati mbili tofauti kwa kupishana muda mfupi. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu nusu ya mji wa Tokyo na kuuwa watu zaidi ya laki moja na elfu hamsini mjini humo.

 Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alizaliwa 20 Oktoba mwaka 1859 na alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri alivyoviandika katika kipindi cha uhai wake ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.

John Dewey

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, wanafunzi kadhaa wa shule za msingi waliwaandikia barua wenzao duniani kote na kuwataka kupitisha muda wao wa siku nzima kwa ajili ya amani. Sehemu moja ya barua ya wanafunzi hao inasomeka kama ifuatavyo: "Wazazi wetu wana imani thabiti na kutupenda, kwa kuwa sisi ni watoto wao. Hata hivyo je, mnafahamu ni dunia ya aina ngani waliyotuandalia? Sisi kamwe tusingekuwa na fursa ya kukua, iwapo wazazi wetu wangefanya kosa japo dogo tu. Tunahitaji suhula kwa ajili ya kukua na malezi." Kwa mnasaba huo, siku ya kwanza ya mwezi Juni kila mwaka, imepewa jina la "Siku ya Watoto Duniani". Kwa hivyo sherehe maalumu hufanyika katika pembe mbalimbali duniani katika kuadhimisha siku hii.