Jun 04, 2021 21:59 UTC
  • Jumamosi tarehe 5 Juni 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Shawwal 1442 Hijria sawa na 5 Juni mwaka 20212.

Na Siku kama ya leo miaka 693 iliyopita alifariki dunia Ibnu Labban faqihi, mpokeaji hadithi, mfasiri wa Qur'ani na mwandishi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 679 Hijria katika mji wa Damascus na kupitisha kipindi cha ujana wake katika mji huo. Ibnu Labban alipata elimu za fiqih, usul-fiqih na hadithi kutoka kwa walimu na maulamaa wakubwa wa zama hizo. Mbali na masomo hayo, Ibnu Labban alikuwa mahiri pia katika kutunga mashairi. Msomi huyo wa Kiislamu alijishughulisha vilevile na kufundisha, kutoa waadhi na kufasiri Qur'an Tukufu. Kitabu pekee kilichochapishwa cha mwanazuoni huyo ni tafsiri ya Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo. Siku kadhaa nyuma, Imam alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo lililouchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni, Imam. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja. Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uiliamua kuwashambulia waandamanaji ambapo uliua na kuwajeruhi wengi kati yao. Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika hapa nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran. Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapo mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza. Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa. Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi tatu zilizotajwa za Kiarabu na kuyashinda kabisa.

Vita vya Waarabu na Israel

Miaka 17 iliyopita Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer. Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni. Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans. Mwaka 1970 aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter. Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ronald Reagan