Jun 05, 2021 22:13 UTC
  • Jumapili tarehe 6 Juni 2021

Leo ni Jumapili tarehe 25 Shawwal 1442 Hijria sawa na Juni 6 mwaka 2021

Siku kama ya leo miaka 1294 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo, miaka 222 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.

Alexander Pushkin

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon. Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kutekeleza jinai mbalimbali dhidi ya wakazi wake. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo likatekeleza mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za sabra nashatila karibu na mji mkuu wa Lebanona, Bairut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu.

Uvamizi wa Israel dhidi ya Beirut

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Juni 1984, jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa la Masingasinga lililojulikana kama Hekalu la Dhahabu katika mjini wa Amritsar makao makuu ya jimbo la Punjab, magharibi mwa India na kuua waasi wa Kisingasinga wasiopungua 1,000. Serikali ya India ilidai kuwa shambulio hilo lilifanywa baada ya kupatikana habari za kufichwa silaha nyingi kwenye hekalu hilo, kwa shabaha ya kuanzisha uasi na mashambulizi dhidi ya serikali kuu. Masingasinga hao nao walilipiza kisasi kwa kumuuwa Indira Ghandi, Waziri Mkuu wa India mwaka huohuo, kiongozi ambaye ndiye aliyetoa amri ya kushambuliwa hekalu hilo.

Hekalu la Dhahabu

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita sawa na tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Jun, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliojawa na huzuni waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht az-Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran. Zaidi ya wananchi na Waislamu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomeini, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye kuelekea eneo la Behesht az-Zahra kwa ajili ya mazishi.

Mahali lilipo kaburi la Imam Khomeini