Jun 07, 2021 21:56 UTC
  • Jumanne tarehe 8 Juni 2021

Leo ni Jumanne tarehe 27 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na Juni 8 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, shirika la kijasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa.  Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.

Atef Bseiso

Tarehe 8 Juni miaka 166 iliyopita, mji wa Lisbon ambao ni mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi elfu arubaini wa mji huo walipoteza maisha yao na theluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngalawa nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba Ureno.

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa unawake taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii.

Na miaka 1101 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (sww) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameandika ya mashairi.

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi