Jun 11, 2021 22:20 UTC
  • Jumamosi tarehe 12 Juni 2021

Leo ni tarehe Mosi Dhilqaada 1442 Hijria sawa na Juni 12 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1269 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya wanahistoria, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko Kaskazini Mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Haram ya Hadhrat Maasuma, Qum

Tarehe 12 Juni miaka 481 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.

Bendera ya China

Tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1964, Nelson Mandela kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alihukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya uhaini dhidi ya mfumo na utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid nchini humo. Mandela alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na wenzake saba akiwemo Walter Sisulu aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha African National Congress kilichokuwa kimepigwa marufuku nchini humo. 

Nelson Mandela

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1975, Indira Gandhi Waziri Mkuu wa wakati huo wa India alizuiwa kuendelea na wadhifa huo kwa miaka sita, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi. Hata hivyo Indira Gandhi alipinga miito iliyomtaka ajiuzulu na akatangaza shjeria za kijeshi kote nchini India baad aya maandamano makubwa ya wananchi yaliyotishia kuiondoa madarakani serikali yake. 

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita inayosadifiana na 12 Juni 1991, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Russia. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Russia kama zilivyokuwa nchi nyingine zilizokuwa zikiunda Umoja wa Kisovieti zilijipatia uhuru wake. Boris Yeltsin aliiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili, hadi mwezi Disemba 1999, alipoamua kung'atuka madarakani.

Bendera ya Russia