Ijumaa tarehe 18 Juni 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na tarehe 18 Juni 2021.
Miaka 726 iliyopita siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa hati na kaligrafia. Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati. Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika nakala ya Qur'ani Tukufu kwa maji ya dhahabu na hati maridadi sana. Nakala hiyo ya Qur'ani na athari nyingine za Ibn Baswis bado ziko hadi leo.

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, vilianza vita vya kihistoria vya Waterloo, vita vya mwisho vya Napoleon Banaparte na madola ya Ulaya. Katika vita hivyo majeshi ya serikali za Prussia na Uingereza yalikutana uso kwa uso na majeshi ya Napoleon Banaparte katika eneo lililokuwa likiitwa kwa jina la Waterloo. Katika vita hivyo na kutokana na kunyesha mvua kali na kuharibika njia zilizokuwa zikitumiwa kwa usafirishaji, hivyo zana za kijeshi zilichelewa kufika uwanja wa vita sambamba na kuchelewa kufika kikosi cha mstari wa mbele cha Wafaransa. Kufuatia hali hiyo, Napoleon Banaparte akawa ameshindwa vibaya katika vita hiyo na hivyo kumfanya akimbie kwa kutumia meli kuelekea kisiwa cha Saint Helena na kufariki dunia miaka kadhaa baadaye kwenye kisiwa hicho.
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, Maxim Gorky, fasihi na mwandishi mashuhuri wa nchini Russia. Alexei Maximovich Peshkov maarufu kwa jna la Gorky, alikuwa mandishi mkubwa aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1868 Miladia katika mji wa Gorky nchini Russia. Alianza kusoma kwa bidii elimu ya fasihi hapo mwaka 1895 na kupewa lakabu ya Maxim Gorky ambayo ilikuja kutumika kama jina lake na baadaye kufikia kupata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kwa kuzingatia kuwa alitokana na familia masikini, hivyo uandishi wa Maxim Gorky ulijikita sana katika kupiga vita umasikini na ujinga. Ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mijeledi Mitatu kinachozungumzia maisha yake.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 utawala wa kifalme ulisambaratika nchini Misri na kukaasisiwa mfumo wa Jamhuri baada ya Mfalme Farouq wa nchi hiyo kupelekwa uhamishoni. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948 wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya Misri kuanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano ya pili ya kupunguza silaha yaliyojulikana kwa jina la Salt 2 kati ya Marais Leonid Brezhnev wa Urusi ya zamani na Jimmy Carter wa Marekani. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kupunguza silaha za nyuklia duniani.
Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, Najmudin Erbakan Waziri Mkuu aliyekuwa na misimamo ya Kiislamu wa Uturuki alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya wanajeshi wa nchi hiyo. Chama cha Erbakan kilipata kura nyingi katika uchaguzi wa Disemba mwaka 1994 na kuunda Baraza la Mawaziri. Lakini wasekulari na makamanda wa jeshi walizuia kutekelezwa malengo ya serikali ya Arbekan. Waziri Mkuu huyo alikuwa akiamini kwamba kuwakandamiza wanaharaki wa Kiislamu nchini Uturuki ni kinyume na demokrasia na alipinga kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel. Lakini Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa wa wanajeshi Februari 1997 lilitoa amri ya kumlazimisha Erbakan akabiliane na wanaharakati wa Kiislamu. Miezi minne baadaye waziri mkuu huyo alishtakiwa mahakamani kutokana na misimamo yake ya Kiislamu na kuzuia kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano.