Jun 18, 2021 22:55 UTC
  • Jummosi tarehe 19 Juni mwaka 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Khordad mwaka 1400 Hijria Shamsiya sawa na 8 Dhulqaada 1442 Hijria Qamariya inayosadifiana na tarehe 19 Juni mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1094 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo. Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa pia cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.

Siku kama ya leo miaka 1063 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran. Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 1057 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar-Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu. Dar-Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kuweza kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Aidha msomi huyo alikuwa hodari pia katika tafsiri ya Qur’an Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘as-Sunan’, ‘Sunan Daru Qutni’ na ‘al-Mukhtalif wal-Mu’talif.’

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Na Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza. Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kuzikomaza fikra za tabaka la vijana. Ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni 'Uislamu na Mwanadamu', 'Historia ya Ustaarabu' na 'Fatima ni Fatima'.