Jun 20, 2021 22:56 UTC
  • Jumatatu tarehe 21 Juni 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na Juni 21 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na 7.3 kwa kipimo cha rishta, na kusababisha maafa makubwa. Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya kuleta maafa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, na hasa kwenye miundombinu.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran.

Dakta Mustafa Chamran

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.

Dakta Ahmed Sukarno

Siku kama ya leo miaka 494 iliyopita aliaga dunia Niccolò Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

Niccolò Machiavelli

Na miaka 616 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo Abu Abdullah Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jina la Sibt al Mardini, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu alizaliwa huko Damascus. Wanahistoria wamesajili vitabu karibu 42 kwa jina la msomi huyo na baadhi ya vitabu hivyo vimehifadhiwa hadi leo hii. Moja kati ya athari za Sibt al Mardini ni kitabu chake cha hisabati kwa jina la Daqaiqul Haqaaiq.

Sibt al Mardini