Alkhamisi tarehe 24 Juni mwaka 2021
Leo ni tarehe 13 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na Jun 24 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 676 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Muhammad Razi. Razi alizaliwa katika eneo la Varamin kwenye viunga vya mji wa Rey na alipata umashuhuri kwa jina la Razi kwa kuwa alikulia katika mji huo. Qutbuddin Muhammad Razi alikuwa mwanafunzi mkubwa wa Allamah Hilli. Kwa kipindi fulani aliwatumikia Sultan Abu Said na waziri wake Khaja Ghiyathuddin Muhammad na aliandika viwili vya 'Sharhu al-Shamsiyyah' na 'Sharhul Matwaali' kwa jina la waziri huyo.' Baada ya kufariki dunia Sultan Abu Said, Qutbuddin Muhammad Razi alielekea Sham na alifariki dunia mjini Damascus.

Siku kama ya leo miaka 414 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Isterabadi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na elimu ya theolojia. Ayatullah Mirza Muhammad Bin Ali Bin Ibrahim Isterabadi alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Awali alikuwa akiiishi mjini Najaf, Iraq na baadaye alielekea Makkah na kufanya makazi mjini hapo. Isterabadi ni kati ya watu wanaoelezwa kuwa waliopata sharafu ya kukutana na Imam wa zama (af). Msomi huyo aliandika vitabu juu ya wapokezi wa hadithi kikiwemo kitabu cha 'Tawdhihul-Maqaal' 'Talkhisul-Aqwaal' na 'Manhajul-Maqaal.' Vitabu hivyo vinatambuliwa kuwa vitabu muhimu na chemchemi ya elimu ya wapokezi wa hadithi.

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.
Tarehe 24 Juni miaka 209 iliyopita, Caracas mji mkuu wa Venezuela ulidhibitiwa na Simon Bolivar wakati wa mapambano ya mpigania uhuru huyo dhidi ya wakoloni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya Amerika ya Kusini. Mkoloni Muhispania alishindwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja na baada ya ushindi huo Simon Bolivar anayejulikana kama shujaa wa mapambano dhidi ya wakoloni huko Amerika Kusini, aliasisi Shirikisho la Colombia Kubwa. Shirikisho hilo lilijumuisha nchi za Venezuela, Colombia, Panama na Ecuador, na Bolivar alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo.
Na siku kama ya leo miaka 178 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.