Jumapili 27 Juni 2021
Leo ni Jumapili tarehe 16 Dhulqaada 1442 Hijria sawa 6 Tir mwaka 1400 Hijria Shamsiya inayosadifiana na Juni 27 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1116 iliyopita alizaliwa Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami katika familia ya Kiirani. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Tarehe 6 Tir miaka 40 iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye wakati huo alikuwa mwakilishi wa Imam Ruhullah Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na pia Imam wa Ijumaa wa Tehran, alinusurika jaribio la kutaka kumuua lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la MKO. Magaidi hao walilipua bomu katika moja ya misikiti ya Tehran ambako Ayatullah Khamenei alikuwa akihutubia hadhara ya watu na kumjeruhi vibaya. Hata hivyo Imam Khamenei alinusurika jaribio hilo kwa njia ya kimiujiza na baadaye akashika usukani wa kuongoza jahazi la Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Ayatullah Ali Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia katika shambulizi hilo.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Djibouti ilipata uhuru baada ya kukoloniwa kwa miaka kadhaa na serikali ya Ufaransa. Djibouti ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tangu mwaka 1896 ikijulikana kwa jina la Somalia ya Ufaransa. Hata hivyo Djibouti hatimaye ilipata uhuru wake baada ya miongo minane ya mapambano. Djibouti ni miongoni mwa nchi za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita Ayatullah Zainul Abidin Mazandarani mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiirani aliaga dunia. Baada ya kuhitimu masomo ya awali, Ayatullah Mazandarani alielekea katika hauza ya kielimu ya Najaf huko Iraq ili kukamilisha masomo ya kidini. Akiwa huko mwanazuoni huyo alifunzwa na maustadhi wakubwa wa zama hizo wa hauza ya Najaf kama vile Sheikh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi.