Jun 27, 2021 22:10 UTC
  • Jumatatu tarehe 28 Juni 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na Juni 28 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1263 iliyopita, Imam Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Imam Kadhim aliwasili Iraq tarehe 7 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 179 Hijria na kufungwa katika jela ya mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Ja'afar aliyekuwa mtawala wa Basra lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabi'i amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun. Hatimaye Imam Kadhim AS aliuawa shahidi na Sindi bin Shahik kwa amri ya Yahya bin Khalid Barmaki ambaye naye alitekeleza amri ya Haroun Rashid. 

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi chuo kikuu cha kidini cha Qum. Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd moja ya miji ya katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza kimasomo ambapo  akiwa huko alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulama maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad. Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo ni chuo kikuu cha kidini katika mji mtakatifu wa Qum. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, Kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza ujenzi huo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini. Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Ratiba na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika kituo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyowafutia sana Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika eneo hilo muhimu. Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kupatwa na wahka na hivyo kusimamisha shughuli zake na hata kukifunga kabisa.

Kituo cha Kiislamu, Washington

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa.

Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein. Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi yake hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake. Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran. 

Na siku kama ya leo miaka 15 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina inayoongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi". Mbali na hayo, mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Mji wa Gaza