Ijumaa, Julai 2, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 21 Dhulqaada 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe Pili Julai mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri. Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani. Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil.
Miaka 96 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."
Tarehe Pili Julai miaka 60 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".
Na tarehe 11 Tir miaka 36 iliyopita Ayatullah Muhamad Saduqi alimu mkubwa, mwanamapambano na Imamu wa Ijumaa wa mji wa Yazd huko katikati mwa Iran, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin na kuwa shahidi wa nne aliyeuawa katika mihrabu ya Swala katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Muhammad Saduqi alikamilisha masomo yake ya kidini katika Hauza ya mji mtakatifu wa Qum, Iran na kustafidi na bahari kubwa ya elimu kutoka kwa walimu mashuhuri wa kituo hicho cha kielimu kama vile Ayatullah Burujerdi na Ayatullah Khansari.