Jumatatu, Julai 5, 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Mfunguo Pili, Dhulqaada 1442 Hijria sawa na Julai 5 mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1242 iliyopita, Imam Ali bin Mussa Ridha (AS) alianza safari kutoka katika mji mtakatifu wa Madina kuelekea Marv, eneo ambalo wakati huo lilikuwa kaskazini mwa Iran ya zamani. Safari hiyo ilifanyika kwa kulazimishwa na kutokana na mashinikizo ya mtawala Maamun, khalifa wa 7 wa utawala wa Kiabbasi, kwa lengo la kumdhibiti mjukuu huyo wa Mtume SAW. Huko Marv, Maamun alimtaka Imam Ridhaa akubali pendekezo la kuwa mrithi wa kiti chake cha ukhalifa. Kiongozi huyo alifanya hivyo ili ajionyeshe kwamba alikuwa mpenzi wa Watu wa Nyumba tukufu ya Bwana Mtume. Hata hivyo Imam alionyesha katika minasaba mbalimbali kwamba hangeshirikiana na utawala wa Bani Abbas na daima aliitambua serikali yao kuwa isiyo halali. Imam Ridha A.S daima alikuwa akifichua na kuweka wazi dhulma na uonevu wa watawala wa Kiabbasi. Baada ya kushindwa kumshawishi Imam Ridhaa, hatimaye Maamun aliamua kumuua shahidi kwa kumpa sumu hapo mwaka 203 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa ajili hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.
Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826 Miladia, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kisayansi katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru dhidi ya wavamizi wa Ufaransa baada ya mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.
Tarehe 14 Tir katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Kalamu. Kalamu huhifadhi elimu na maarifa na ni mlinzi wa fikra za wasomi na wanafikra, kiunganishi cha kifikra na daraja la mawasiliano baina ya watu wa zamani na wa leo. Hata mawasiliano baina ya mbingu na ardhi yamepatikana kupitia kalamu. Kwa msingi huo, kalamu ni mtunza siri wa mwanadamu na hazina ya elimu na mkusanyaji wa tajiriba za karne nyingi. Katika Qur’ani pia Mwenyezi Mungu ameapa kwa kalamu kwa kusema: Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo. Kiapo cha Mwenyezi Mungu kwa kutumia kalamu kinaonesha umuhimu wa wenzo huo, kwani kiapo mara nyingi hufanywa kwa jambo au kitu ambacho kina thamani na heshima kubwa.
