Jumanne tarehe 6 Julai 2021
Leo ni Jumanne tarehe 25 Mfunguo Pili Dhulqaada 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Julai 2021.
Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita Nabii Muhammad (saw) aliondoka Madina akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja na kuelekea Makka kwa ajili ya kutufu nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba. Tangu alipohamia Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kutufu al Kaaba lakini alifanikiwa mara mbili tu kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija, Mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada ya Hija kwa njia sahihi. Baada ya kukamilisha ibada hiyo, Mtume Muhammad (saw) alirejea Madina na alipofika katika eneo la Ghadir Khum aliwakusanya masahaba zake, na kwa amri ya Mola wake alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na Kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Katika siku kama ya leo miaka 167 iliyopita alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na alivutiwa sana somo la fizikia. Alifanikiwa kuvumbua kanuni ya umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni hizo zinatumiwa hadi leo hii.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na Tanzania, Zambia na Msumbiji.
Tarehe 6 Julai miaka 46 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12.Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 ma inapatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika Bahari ya Hindi.
Na katika siku kama hii ya leo miaka 35 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Jawad Khamenei, baba wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Alizaliwa mwaka 1313 Hijria katika eneo la Khamene karibu na Tabriz mkoa wa Azarbaijan Mashariki, na katika kipindi cha ujana wake alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had kwa ajili ya kutafuta elimu na maarifa. Akiwa huko alihudhuria darsa wa Ayatullah Aghazadeh Khorasani na Haj Agha Hussein Qummi na kukwea haraka daraja za juu za elimu. Mwaka 1305 Hijria Shamsia alielekea Najaf nchini Iraq na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo mtukufu kama Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abulhasan Isfahani. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia tarehe 15 Tir miaka 35 iliyopita akiwa na umri wa miaka 91 baada ya maisha ya zuhudi na uchamungu. Ayatullah Jawad Khamenei alizikwa katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Mussa al Ridha (as) katika mji wa Mash'had.