Jumatano tarehe 7 Julai 2021
Leo ni Jumatano tarehe 26 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na Julai 7 mwaka 2021.
Miaka 720 iliyopita sawa na leo, alizaliwa faqihi, mfasiri, mtaalamu wa itikadi na mwanafasihi wa Kiislamu Masud bin Omar Taftazani huko katika eneo la Quchan kaskazini mwa Iran. Kwa kipindi kirefu cha umri wake Masud Taftazani alifanya safari katika miji ya Khorasan na Asia ya Kati kwa lengo la kutafuta elimu na maarifa. Allamah Taftazani alianza kuandika na kutunga vitabu akiwa bado kijana wa miaka 16 kutokana na umahiri wake mkubwa na baadhi ya vitabu vyake vinatumiwa kufundishia hadi hii leo. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Mutawwal, al Irshad na Mukhtasarul Maani. Allamah Taftazani aliaga dunia mwaka 792 Hijria katika mji wa Samarkand.
Miaka 214 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, ulidumu hadi mwaka 1810.
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, yaani tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Rabbani Zainul Abidin Marandi. Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlid katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadil-Salaam mjini Najaf.
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi, msomi mkubwa wa fiqhi na masomo mengine ya kidini. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya kidini yapata mwaka 1281 Hijiria Shamsia, ambapo aliweza kusoma masomo ya ngazi ya juu ya usulu fiqhi na fiqhi kwa maulama wakubwa wa mji huo kama vile Ayatullah Akhund Mohammad Kazem Khorasani na Mohammed Kazem Yazdi. Aidha Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi ameandika vitabu kadhaa kama vile 'Kifaayatul-Usul' 'al-Badrut-Tamaam' 'Zallatul-Aqdaam' na 'al-Fawaaidur-Rijaaliyah.'
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru. Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu. Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.
Na tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa. Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo. Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.