Jul 08, 2021 23:16 UTC
  • Ijumaa tarehe 9 Julai 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Dhulqaada 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Julai 2021.

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.

Miaka 19 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika.

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo njama ya mapinduzi ya Nojeh iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani nchini Iran iligunduliwa na kuzimwa. Njama hiyo ya mapinduzi iliratibiwa na Shirika la ujasusi la Marekani (CIA) likishirikiana na baadhi ya vibaraka wa jeshi la anga la utawala wa Shah kwa shabaha ya kumuua Imam Khomeini, kuangamiza utawala wa Kiislamu hapa nchini na kumrejesha madarakani  Shapur Bakhitiyar. Waratibu wa njama hiyo ya mapinduzi walikusudia kufanya mashambulizi dhidi ya makazi ya Imam Khomeini mjini Tehran na kumuua na kisha kushambulia kituo cha kuongozea ndege cha uwanja wa Mehrabad. Hata hivyo njama hiyo iligunduliwa na kusambaratishwa na waratibu wa njama hiyo walitiwa mbaroni na kuhukumiwa.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita na baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena. Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.

Na tarehe 28 Dhilqaada miaka 1082 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya hadithi za Mtume (saw). Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya utafiti na uchunguzi wa miaka 33.

Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya hadithi kwa majina ya Al Muujamul Kabiir", al Muujamul Ausat na al Muujamu Swaghir.