Jul 16, 2021 00:13 UTC
  • Ijumaa tarehe 16 Julai 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Mfunguo Tatu Dhulhija 1442 Hijria sawa na Julai 16 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

James Parkinson

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alifariki dunia huko Najaf, Iraq Allamah Muhammad Hussein Kampani, mwanafalsafa, faqihi na mwanairfani mkubwa. Alizaliwa mwaka 1296 Hijria mjini Kadhimain nchini Iraq. Msomi huyo mkubwa alitabahari katika elimu za falsafa, tiba, irfan, historia, jiografia, mashairi na fasihi. Mbali na hayo Allamah Hussein Kampani alikuwa na fikra pevu na uwezo mkubwa wa kubainisha mambo. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa katika nyanja mbalimbali ikiwemo diwani ya mashairi akisifu viongozi wa Uislamu.

Allamah Muhammad Hussein Kampani

Miaka 76 iliyopita katika siku kama hii ya leo bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa kukabidhi mabaki ya maiti za askari wawili wa Kizayuni. Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantwari ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.

Samir Qantari