Jul 24, 2021 04:39 UTC
  • Jumamosi, 24 Julai, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1442 Hijria mwafaka na tarehe 24 Julai 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 238 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia. Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.***

Simón Bolívar

 

Miaka 219 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa. ***

Katika siku kama ya leo

Alexandre Dumas

 

miaka 104 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran. Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza. Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni. ***

Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi,

 

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo. ***

 

Miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo. Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi. ***

Mashambulio ya mabomu dhidi ya bandari ya Hamburg

 

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah, maulamaa kadhaa na marajii kutoka Qum na Mash'had na miji mingine ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran. Mbali na kuandika barua wakithibitisha daraja ya Umarjaa ya Imam Khomeini walitoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo. Hatua hiyo sambamba na kuendelea upinzani wa wananchi dhidi ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kuliulazimisha utawala wa Shah kumhamisha kiongozi huyo kutoka jela na kumpeleka katika nyumba moja ili kuwatuliza maulama na wananchi hao. Siasa hizo za kutuliza mambo hazikuwa na taathira na kwa msingi huo utawala wa Shah ukiwa na lengo la kuweka pengo baina ya Imam Khomeini na wafuasi wake, uliamua kumbaidishia mwanazuoni huo nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye nchini Iraq. ***

Imam Khomeini

 

Na tarehe 13 Dhulhija miaka 53 iliyopita alifafriki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. ***

Allamah Agha Bozorge Tehrani (wa katikati)