Aug 07, 2021 01:07 UTC
  • Jumamosi, 7 Agosti, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 7 Agosti 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 751 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz nchini Iran, akiwa kijana Saadi Shirazi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na katika maeneo mengine. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan. ***

Saadi Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita sawa na Agosti 7 1960 nchi ya Ivory Coast ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno waliidhibiti nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika katika karne ya 16, lakini ulipofika mwaka 1891 Ufaransa iliidhibiti nchi hiyo, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wa Ivory Coast. Hatimaye ulipofika mwaka 1960, Ivory Coast ikiwa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika zilizokoloniwa na Mfaransa zilijipatia uhuru wao. ***

Bendera ya Ivory Coast

 

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, yalitiwa saini makubalino ya kuondoka vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) mjini Beirut Lebanon kati ya Marekani, Lebanon na PLO. Makubaliano hayo yalitiwa saini kufuatia shambulio kubwa lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon mwezi Juni 1982 kwa shabaha ya kuwafukuza wapiganaji wa PLO nchini Lebanon. Ijapokuwa kuondoka wanaharakati wa PLO nchini Lebanon kulitoa pigo kubwa kwa harakati hiyo, lakini miaka ya baadaye Wazayuni maghasibu walikabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa harakati ya muqawamah ya Lebanon, na kulazimika kuondoka kwa madhila katika ardhi ya nchi hiyo mwaka 2000. ***

Yassir Arafat, kiongozi wa zamani wa PLO

 

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo. Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.***

Georgia