Sep 10, 2021 02:45 UTC
  • Ijumaa,10 Septemba, 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 10 mwaka 2021

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Miaka 107 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya ziwa la Mazury. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi waitifaki. Katika vita hivyo vya Mazury, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walifanikiwa kupata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Ziwa la Mazury

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi lilisababisha mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 kuangamia na watu 10,000 kupoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo vilevile ulitoa pigo kubwa kwa miundo mbinu ya uchumi wa nchi hiyo.

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.

Sayyid Mahmoud Talaqani

Na tarehe 10 Septemba mwaka 1990 Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi. Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu karibu laki mbili na nusu.

Samuel Kanyon Doe