Oct 08, 2021 02:23 UTC
  • Ijumaa tarehe 8 Oktoba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 8 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume (saw) na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba ilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1378 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein (as) pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein (as) aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania. Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake. Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo.

Miaka 93 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya udikteta wa Reza Khan Pahlawi, mtawala huyo aliwaamuru askari wake wavamia nyumba ya Ayatullah Muddares, kumpiga na kumjeruhi na kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran. Askari hao pia waliwatia nguvuni watu wa familia ya mwanazuoni huyo. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Reza Khan mwaka 1316 Hijiria Shamsia.

Sayyid Hassan Mudarres

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita sawa na tarehe 8 Oktoba 1990 kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel ulifanya jinai ya kinyama kwa kuwashambulia waumini wa Kipalestina waliokuwa wakiswali ndani ya Msikiti mtukufu wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wapalestina 20 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa. Mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel tena ndani ya Msikiti wa al-Aqsa, kwa mara nyingine tena yalilipua ghadhabu za fikra za walio wengi duniani dhidi ya utawala huo katili. Hata hivyo kama kawaida uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ulizuia kuchukuliwa hatua zozote za kivitendo dhidi ya utawala huo.

Miaka 16 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu wapatao 90 elfu walipoteza maisha yao na wengine milioni 3 na laki 6 kubaki bila makazi kufuatia mtetemeko huo.

 

Tags