Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (29) +SAUTI
Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Ahmad bin Muhammad Ardabili mashuhuri zaidi kwa jina la Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili. Tulisema kuwa, Ahmad bin Muhammad Ardabili maarufu kama Muqaddas Ardabili ni mmoja wa Maulamaa wakubwa na mashuhuri katika Ulimwengu wa Kishia katika karne ya 10 Hijria. Sehemu ya 29 ya mfululizo huu juma hili itaendelea na maudhui hii. Karibuni.
Muqaddas Ardabili kutokana na kujipamba kwake na taqwa na ukarimu mwingi ulioonekana na watu kwake, aliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Muqaddas. Inanukuliwa kwamba, alimu huyo mkubwa wa Kishia katika kipindi chote cha miaka 40 siyo tu kwamba, hakutenda dhambi, bali hakufanya hata jambo ambalo ni makuruhu yaani lisilopendeza.
Siku moja, Bwana mmoja alimng’ang’ania Muqaddas Ardabili na kumuuliza, hivi ni kweli wewe hutendi dhambi? Katika kujibu swali hilo alimu huyo alisema: Kwani wewe unakula najisi, au hata uko tayari kukaa na kuitazama? Mtazamo wetu kuhusiana na dhambi uko namna hii.
Wanazuoni na wasomi wengi wakubwa wa dini wanashuhudia kwamba, Muqaddas Ardabili alikuwa amefikia daraja ya juu mno ya uchaji Mungu, ibada na kuipa mgongo dunia na hakuwa na mithili katika zama zake. Katika zama zake, alimu huyo alikuwa ndiye mcha Mungu zaidi, mwenye kumuabudu zaidi Mwenyezi Mungu na mwenye kumuogopa zaidi Mola Muumba, kiasi kwamba, watu wa kawaida walikuwa wakimpigia mfano wa taqwa na utukufu.
Muqaddas Ardabili mbali na kuwa dhihirisho la utakasifu na utukufu, hakuwa mfano na kigezo cha watu wa kawaida tu bali hata Maulamaa wa dini katika tabia njema na ukarimu. Kuna nukuu na simulizi nyingi zinazoelezewa kuhusiana na tawadhui, unyenyekevu, subira, ukarimu, moyo wa kutoa na kuwa mtu wa watu kuhusiana na Muqaddas Ardabili ambapo kusikiliza simulizi hizo kunaweza kumsaidia mtu kutambua vilele vya utu na ubinadamu.
Inasimuliwa kwamba, alimu na mwanazuoni huyu alipokuwa akiletewa zawadi ziwe ni zenye thamani ndogo au kubwa alikuwa akizipokea zote. Wakati mwingine alikuwa akiletewa vitambaa vya ghali na vyenye thamani kubwa ambavyo vilikuwa na thamani ya dhahabu na Sheikh alikuwa na mazoea ya kujifunga kitambaa kama kilemba na kisha kutoka nje. Anapokuwa njia na alipokuwa akimuona masikini au fakiri alikuwa akitenganisha sehemu ya kilemba na kumpatia masikini au fakiri, kiasi kwamba, mpaka anarejea nyumbani hakuwa na kitu kichwani isipokuwa sehemu ndogo ya kufunika kichwa.
Kusamehe na ukarimu ni sifa alizojipamba nazo Muqaddas Ardabili kiasi kwamba, watu walikuwa wakimfananisha na Hatim Tai aliyekuwa mashuuhuri kwa ukarimu. Katika kipindi cha ukame, Muqaddas Ardabili alikuwa akitoa kila alichokuwa nacho ndani ya nyumba na kukigawa baina ya masikini na alikuwa akibakisha kwa ajili ya familia kiwango cha sawa na hisa ya masikini wake. Siku moja mke wake alimlalamikia na kuonyesha wasiwasi wa kubakia watoto na njaa. Muqaddas Ardabili alitoka ndani ya nyumba na kwenda nje bila ya kumjibu mkewe. Alipotoka nyumbani alielekea katika msikiti wa Kufa kwa ajili ya ibada ya itikafu. Zikapita siku mbili tangu alimu huyo aondoke nyumbani kwake, ambapo Bwana mmoja ambaye hakuna aliyekuwa akimjua alikwenda nyumbani kwa Muqaddas Ardabili akiwa na ngano nyingi pamoja na unga mzuri na kuiambia familia ya Sheikh kwamba, vitu hivi nimepatiwa na Sheikh nikuleteeni kwani yeye yuko katika itikafu. Baada ya Muqaddas Ardabili kurejea nyumbani, mkewe alionyesha kuridhishwa mno na ule unga wa ngano mzuri. Muqaddas Ardabili ambaye hakuwa na habari ya vitu hivyo na wala hakuvituma yeye, alifahamu kwamba, hiyo ilikuwa ni atia na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo akanyanyua mikono na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Tawadhui na unyenyekevu ni sifa nyingine ambayo alijipamba nayo Muqaddas Ardabili na alitambulika pia kwa sifa hiyo. Inasimuliwa kwamba, siku moja msafara ulikuwa ukipita katika mji wa Najaf na ulikuwa na nia ya kupumzika katika mji huo mtakatifu. Mmoja wa watu wa msafara huo aliyekuwa amechoka na huku akiwa ametapakaa vumbi, alimuona Muqaddas Ardabili hata hivyo hakumtambua. Bwana yule alimtaka Muqaddas Ardabili amfulie nguo zake zile zilizokuwa zimejaa vumbi na kwamba angemlipa ujira kwa kazi hiyo. Muqaddas Ardabili alikubali na akachukua nguo zile na kuanza kuzifua. Akiwa anaendelea na kazi yake, mtu mmoja alimtambua Sheikh na akamlaumu mno Bwana aliyempatia nguo Sheikh ili azifue. Bwana yule akiwa ametahayari na uso ukiwa umejaa soni na aibu, alimtaka radhi Muqaddas Ardabili. Hata hivyo alimu huyo akiwa mtulivu na mpole hali ya kuwa anatabasamu alisema: Haki ya muumini kwa ndugu yake muumini ni zaidi ya kumfulia nguo. Kwa nini unanitaka radhi?
Katika kipindi chote cha umri na uwezo wake, mwanzuoni huyo alifanya huduma kubwa tena kwa ikhlasi kwa maktaba ya Ahlul-Baiti (as) na ni miongoni mwa watu wachache waliopata fursa ya kukutana na kuzungumza na Imam wa Zama, Imam Mahdi (atfs).

Mmoja wa wanafunzi wa Muqaddas Ardabili aliyejulikana kwa jina la Mir Feidhullah Tafrashi anasimulia kwamba: Usiku mmoja baada ya kumaliza kujisomea, nilikuwa nimekaa chumbani kwangu. Chumba changu kilikuwa kimeelekea Haram ya Amirul-Muuminina (as) mjini Najaf. Ukiwa ni usiku wa manane, mara nikamuona mtu anaelekea upande wa Haram. Nilidhani huenda akawa mwizi, hivyo, nikaamua kumfuatilia. Baadaye nikafamu kwamba, ni mwalimu wangu Muqaddas Ardabili. Alipokaribia kaburi tukufu, milango na kufuli zikafunguka. Nikaingiwa na udadisi zaidi hivyo nikaendelea kumfuatilia taratibu.
Sheikh akaja na kusimama mbele ya kaburi tukufu na nikawa nasikia anazungumza na mtu. Kisha akatoka na kuelekea katika mji wa Kufa. Nikamfuata. Ndani ya msikiti wa Kufa jirani na mehrabu alizungumza kwa muda mrefu na mtu ambaye sikuwa nikimfahamu na kisha akarejea. Hapo ndipo Sheikh alifahamu kwamba, namfuata. Nikamtaka anieleze kilichojiri na kwamba, alikuwa akizungumza na nani. Hata hivyo Sheikh alikataa katakata. Binafsi niliendelea kumng’ang’ania na kumtafadhalisha anieleze. Hatimaye Sheikh akasalimu amri lakini akataka ahadi kutoka kwangu kwamba, atanieleza kwa sharti kwamba, nisimsimulie mtu yeyote katika kipindi cha uhai wake. Nikamuahidi kufanya hivyo. Muqaddas Ardabili akasema: Kulikuwa na mas’ala ya kidini ambayo ilinishinda. Hivyo nikaenda kwa Amirul-Muuminina ili nikamuulize. Hata hivyo, Amirul-Muumina akaniambia kwamba, leo Imam wa Zama atakuwa katika Msikiti wa Kufa hivyo, nenda huko na ukamuulize swali lako. Hivyo nikaenda na nikamuuliza mas’ala iliyokuwa ikinisumbua na yeye akanipatia jibu lake. Yule mtu uliyemuona ninazungumza naye katika mehrabu ya Msikiti wa Kufa ni Imam wa Zama, Imam Mahdi (atfs).
Ndio katika ulimwengu huu huu uliojaa giza kuna shakhsia wakubwa ambao kupitia taqwa na uchaji Mungu wao wanafikia chanzo cha nuru na kupata saada hapa duniani na Akhera. Hatiamye alimu na msomi huyu aliaga dunia mwezi Rajab 993 Hijria na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) mjini Najaf Iraq.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.