May 23, 2016 09:53 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (42)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni tena kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kuwafanyia wema na hisani watu wengine ni miongoni mwa vitendo vizuri na kinachosifiwa na ambacho kinaungwa mkono na akili na ada za kijamii.

Tab’ani kuwatendea wema na hisani wazazi yaani baba na mama ni jambo lenye umuhimu mkubwa zaidi. Katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 42 ya mfululizo huu tutazungumzia maudhui hii na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na kuwatendea wema wazazi wawili. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo. 

*********

Kuwatendea wema na hisani baba na mama na na kuishi nao kwa heshima na adabu ni miongoni mwa vitendo ambavyo ni chimbuko la saada na ufanisi wa mwanadamu hapa duniani na kesho akhera

Mweyezi Mungu anasema katika aya ya 15 ya Surat al-Ahqaaf:

Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thelathini. Hata anapofika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu…

Katika kufasiri aya hii, Allama Tabatabai mfasiri mkubwa wa Qur’ani anasema:

Natija ya ombi la mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu ni kupata ilhamu katika moyo wake ya kushukuru neema za Allah Muumba na kutenda amali njema na kuwatendea wema baba na mama, kutengenezewa dhuria zake na vile vile watoto wake wamheshimu kama yeye alivyokuwa akiwaheshimu wazazi wake.

Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 23 na 24 za Surat al-Israa:

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.

*********

Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Zakaria anasimulia kwa kusema:

Nilikuwa Mkristo ambaye nimesilimu na kuingia katika Uislamu na nikapata fursa na uwezo wa kwenda kuhiji. Nikiwa katika mji wa Madina nilimtembelea Imam Ja’afar Swadiq (a.s). Baada ya kujitambulisha na kumueleza Imam kwamba, mimi kabla nilikuwa Mkristo na sasa nimesilimu na kuwa Mwislamu nilimuuliza. Baba na mama yangu ni Wakristo na mama yangu ni kipofu na mimi ninaishi nao na hivyo ninakula nao pamoja je kufanya hivi kuna mushkili? Imam Ja’afar Swadiq AS akaniuliza, je wazazi wako wanakula nyama ya nguruwe? Nikamjibu kwa kumwambia, hapana. Imam AS akasema, basi hakuna tatizo kula chakula pamoja na mama yako. Mtendee wema zaidi na kama atafariki dunia wewe mnwenyewe shughulikia suala la mazishi yake.

Bwana huyo anaendelea kusimulia akisema kuwa, baada ya kumalizika msimu wa ibada ya Hija nilirejea mjini Kufa na nikawa namfanyia wema na huruma mama yangu kama alivyoniusia Imam Swadiq AS. Hivyo nikawa nikimfulia ngua zake na kumuosha nywele zake na kumhudumia kwa huruma na upole wa hali ya juu. Siku moja mama yangu akaniuliza, mwanangu, ulipokuwa Mkristo hukuwa ukinifanyia mapenzi namna hii, sasa umekuwa Mwislamu unaniheshimu na kunihudumia zaidi. Nikamwambia, hizi ni nasaha za mmoja wa watoto wa Mtume wetu.

Mama yangu akauliza? Je yeye ni Mtume? Nikamwambia hapana, yeye ni mmoja wa wajuu wa mtukufu huyo. Kisha mama yangu akasema, dini yako ni dini iliyo bora kabisa, nifundishe na mimi niwe Mwislamu. Nikamfundisha mama yangu kutamka shahada mbili na namna ya kuswali. Mama yangu akaswali Swala za Adhuhuri na Alasiri, Magharibi na Isha na kisha usiku huo huo hali yake ikawa mbaya. Akaniita na kuniambia nimkaririe yale niliyomfundisha, nami nikafanya kama alivyotaka. Kisha usiku huo huo, mama yangu akaaga dunia. Kulipokucha Waislamu walikusanyika na baada ya mwili wake kuoshwa nikamswalia na kama alivyoniusia Imam Ja’afar Swadiq nikaingia kaburini mwenyewe na kumzika mama yangu.”

Dini ya Kiislamu ni miongoni mwa dini ambazo zimempa heshima kubwa baba na mama huku ikimpa nafasi ya hali ya juu kabisa mama. Katika Qur’ani Tukufu Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 14 ya Surat Luqman

 “Na tumemuusia mwanadamu kwa ajili ya wazazi wake, mama yake amembeba kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha kunyonya katika miaka miwili kwamba, unishukuru mimi na wazazi wako, marudio (ya mwisho) ni kwangu.”

Aya hii tukufu inamuusia mwanadamu kuwatendea wema baba na mama yake, na wakati huo huo kumpa nafasi maalumu mama kutokana na mateso na taabu ya hali ya juu anayoipata katika kipindi cha ujauzito wake. Katika kipindi cha ujauzito, mama hujitolea maisha yake yote yaliyojaa mapenzi kwa ajili ya kulea kitoto chake kilichoko tumboni na baada ya kuzaliwa hukinyonyesha maziwa yake kwa muda wa miaka miwili mtawalia tena kwa huba na mapenzi ya hali ya juu.

*********

Katika Qur’ani Mwenyezi Mungu ameamrisha mara 23 moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusiana na kuwatendea wema baba na mama. Katika aya ya 23 ya Surat al-Israa Mwenyezi Mungu anakataza kufanyiwa ukosefu wa adabu baba na mama hata uwe mdogo kiasi gani. Aya hiyo inamtaka mtu kutomtamkia mzazi wake hata neno dogo zaidi la dharau na kuwakosea heshima ambalo ni Akh!. Neno Akh! Ni neno au ibara ya kiwango cha chini zaidi cha ukosefu wa adabu ambayo hutumika pale mtu anapokuwa na hasira au kuchukizwa na jambo fulani. Qur'ani Tukufu inamkataza mwanadamu kutumia neno lolote dogo kiasi hicho au harakati yoyote ndogo ambayo inaweza kuwaletea maumivu ya moyo wazazi wake wawili. Qur'ani Tukufu pia inabainisha tabia na mienendo bora inayotakiwa kufanywa na watoto kuhusiana na wazazi wao.

Imam Swadiq AS anasema kuwa, kama kungekuwa na kitu kidogo zaidi ya aah, basi Mwenyezi Mungu angekikataza na neno hili ndilo dogo zaidi katika kupinga na kuonesha mtu ukosefu wa adabu kwa baba na mama.

Mtume SAW alimjibu bwana mmoja aliyemuuliza kuhusu haki za wazazi kwamba:

Baba na mama ni pepo na Jahanamu yako. Pepo katika ridhaa yao na Jahanamu katika hasira na ghadhabu zao.

Maneno haya yanaonesha kwamba, endapo mtu ataridhiwa na kupata radhi ya wazazi basi ataingia peponi lakini kama atawaudhi wazazi wake na kuwafanya wamghadhibikie, bila shaka ataingia katika moto wa Jahanamu.

Kuhusiana na athari za muamala mzuri na kuwatendea wema wazazi kuna hadithi nyingi zilizopokewa katika uwanja huo.

Moja ya hadithi hizo ni ile iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW ambapo anawasisitizia wafuasi wake kwa kusema;

Kila ambaye anapenda umri wake uwe mrefu, riziki yake iwe nyingi, mambo yake yamuendee vizuri na kumnyookea, astaladhi na maisha yake na watoto wake wamheshimu, basi anapaswa kuwaheshimu baba na mama yake, kwani kitendo hiki ni katika kumtii Mwenyezi Mungu.

Imam Muhammad Baqir AS anasema kuwa, kuwafanyia hisani na kuwatendea wema baba na mama kunaondoa umasikini na madhila na kumuepusha mtu na aina sabini ya vifo vibaya.

Muda wa kipindi hiki kwa leo umemalizika wapenzi wasikilizaji, tukutane wiki ijayo.