Jumamosi, 13 Novemba, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1443 Hijria mwafaka na tarehe 13 Novemba 2021 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Abul-Feidh Hamdun Ibn Abdul-Rahman mashuhuri kwa jina la Ibn Haj, mfasiri, mwanafasihi na fakihi wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1174 Hijria katika moja ya miji ya leo ya Morocco na kukulia huko. Ibn Abdul-Rahman alisoma elimu za fasihi na dini kwa walimu na maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Alimu na mwanazuoni huyu alikuwa mahiri pia katika uandishi wa vitabu ambapo ana vitabu mbalimbali katika elimu za fikihi, teolojia, tafsiri, mantiki na elimu nyigine. ***

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh kaka wa Imam Ruhullah Khomeini. Alisoma masomo ya awali ya kidini kwa maulama na wanazuoni wa mji wa Isfahan na kushiriki masomo ya elimuu ya juu ya kidini kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Baadaye alirejea katika mji wa Khomein na kujishuhulisha na ufundishaji wa fikihi, usuul na masomo mengine. Ayatullah Pasandideh anayejulikana kama alimu na mujahidi, kipindi fulani alibaidishwa kutokana na upinzani wake kwa utawala wa kifalme wa wakati huo wa Reza Khan na kusimama kwake kidete dhidi ya utawala huo. ***

Na miaka 6 iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya Kati milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika maeneo nambari 1, 10 na 11 ya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368. Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris. Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo. ***
