Jumanne tarehe 16 Novemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 10 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Novemba 16 mwaka 2021.
Miaka 1242 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as). Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.

Tarehe 10 Rabiuthani mwaka 1330 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 113 iliyopita Haramu tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridhaa, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran. Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao.

Miaka 41 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam. Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.
Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Allama Muhammad Taqi Jaafari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekkana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi. Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Jaafari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahaj al-Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo.

Na miaka 21 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, na katika kipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf, Iraq akiwa pamoja na baba yake, Allama Amini, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri. Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki.