Ijumaa tarehe 19 Novemba 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na tarehe 19 Novemba 2021.
Siku kama ya leo miaka 1224 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu na fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw).
Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, alifariki dunia Franz Schubert mtunzi wa nyimbo maarufu wa nchini Austria. Schubert alizaliwa mwaka 1797 katika familia masikini. Tangu akiwa kijana mdogo alipendelea sana nyimbo huku akiwa na kipawa kikubwa katika uwanja huo na hivyo kuamua kusomea taaluma hiyo. Alianza kubuni nyimbo akiwa kijana na katika umri wake wote aliimba zaidi ya nyimbo 600. Hata hivyo licha ya kuimba nyimbo nyingi hususan mziki wa asili, bado hakuweza kujinasua kutoka kwenye umasikini. Hii ni kwa kuwa nyimbo zake hazikupokelewa kwa wingi na jamii ya wakati wake. Ni baada ya kufariki dunia ndipo nyimbo zake zikapewa umuhimu mkubwa katika jamii.
Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko Allah Abadi nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa.
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari katika Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Sadat ambayo pia ilizusha machafuko na ghasia nchini Misri kwenyewe. Hatimaye mwaka 1981 Khalid Islambuli aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri alimpiga risasi na kumuua Sadat akipinga hatua yake ya kutia saini mkataba muovu wa Camp David.
Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, viongozi wa Jumuiya za Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) na Warsaw walitiliana saini maafikiano ya usalama mjini Paris, Ufaransa. Mkataba huo ulihitimisha vita baridi baina ya kambi mbili za Magharibi na Mashariki. Viongozi wa kambi hizo pia walikubaliana kumaliza vita vya propaganda kati yao na kupunguza silaha za jumuiya mbili hizo za kijeshi.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam lililokuwa likiongozwa na gaidi Msaudi Arabia, Majid al Majid ambalo ni miongoni mwa matawi ya kundi la kigaidi la al Qaida, lilishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran mjini Beirut huko Lebanon kwa kutumia magaidi wawili waliojilipua kwa mabomu. Katika mashambulizi hayo mawili ya kigaidi watu 23, akiwemo Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari aliyekuwa Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran nchini Lebanon na mke wa mmoja kati ya wanadiplomasia wa Iran, waliuawa shahidi na watu wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa. Walinzi wanne wa ubalozi wa Iran mjini Beirut pia waliuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Majid al Majid alitiwa nguvuni lakini aliuawa kwa njia ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi mjini Beirut kabla ya kutoa taarifa yoyote na maiti yake ikakabidhiwa kwa maafisa wa utawala wa Saudi Arabia.
