Nov 20, 2021 07:19 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (33)

Assalaam alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote mlipo

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari maisha ya alimu na msomi mwingine mashuhuri wa Kishia yaani  Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad mwanafalsafa mkubwa wa Kishia. Tulisema kuwa, Mir Mohammad ni mwanafalsafa mkubwa, mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mshairi mahiri wa Kishia. Tulieleza pia kwamba, akiwa ameazimia kutekeleza malengo yake makubwa ya uhakiki, Mir Damad alifunga safari na kuelekea katika miji ya Qazvin, Harat na Isfahan ambayo katika zama hizo kila moja kati ya miji hiyo kilikuwa kituo muhimu cha elimu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 33 kitaendelea kumzungumzia msomi huyu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Katika karne ya 11 falsafa ya Kiislamu ilipiga hatua kubwa na ya kuzingatiwa na baadhi ya wanazuoni na wasomi wakubwa wa Kishia waliliweka suala la falsafa katika uga wa harakati zao. Hii kwamba, kwa nini Maulamaa wa Kiislamu waliingia katika uga wa falsafa kuna sababu mbalimbali kuhusiana na hilo.  Moja ya sababu hizo inafungamana na utambulisho wa elimu ya falsafa. Falsafa kwa maana ya tafakuri kuhusiana na maudhui jumla na za kimsingi zaidi katika maisha na katika ulimwengu ambazo tunakumbana nazo.

 

Falsafa hujitokeza pale  tunapojiuliza maswali ya kimsingi kuhusiana na sisi wenyewe pamoja na ulimwengu kwa ujumla. Maswali kama: Kabla ya kuzaliwa tulikuwa wapi na baada ya kifo nini kitatupata? Uzuri na ujamali ni nini? Je maisha yetu yanaongozwa na kusimamiwa na mtu au nguvu nyingine? Je ulimwengu unahitajia muumba? Lengo la maisha ni nini? Saada na ufanisi wa kweli ni nini? Na makumi ya maswali mengine mfano wa haya. Hivyo basi wanafalsafa wanafanya hima na juhudi za kujibu maswali haya kwa kutegemea akili. Hata hivyo kwa kuwa makini kidogo tutaona kuwa, maswali haya ndio yale maswali ya kimsingi ambayo dini za mbinguni zinayajibu.

Miongoni mwa dini mbalimbali, dini ya Uislamu na hususan madhehebu ya Shia, kutokana na umuhimu inaotoa kwa akili na utumiaji akili, yananasibiana zaidi na elimu ya falsafa. Utambulisho wa tafakuri na fikra ya Kiislamu hususan fikra ya Kishia, inaoana na kushabihiana na akili na kutumia akili pamoja na mafundisho muhimu ya Uislamu ikiwemo Qur’ani na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maasumina (a.s) ambazo zinasisitiza na kukokoteza kuhusu suala la kutumia akili kwa njia sahihi na kufuata hukumu za kiakili.

 

Katika mafundisho ya Uislamu akili ipo kando ya Wahyi, hoja na muongozo ambao Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu ili kwa kutumia hayo aweze kupata njia ya hidaya na uongofu. Kitabu cha Nahaj al-Balagha (Njia ya Balagha) ambacho ni mkusanyiko, majimui na mjumuiko teule uliokusanya humo hotuba, mawaidha, nasaha, barua, mikataba, semi, maneno na jumbe fupi fupi za Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (a.s), humo kunapatikana hotuba na maneno mengi ya Kifalsafa na Kiirfani ya Imam huyo wa mashariki na Magharibi. Aidha kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu wengine watoharifu (a.s) hususan Maimamu Muhammad Baqir (a.s), Jaafar Swadiq pamoja na midahalo ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) ambayo imejaa hoja za kiakili na kifalsafa. Kwa msingi huo basi, hakuna wakati ambao utambulisho wa kifikra wa Ushia ulikuwa tupu na fikra pamoja na mitazamo ya Kifalsafa.

 

Katika upande mwingine katika zama zile Maulamaa wa Kishia walikuwa wakikabiliwa na tukio jingine jipya nalo ni kukabiliana na ustaarabu wa Kimagharibi. Katika zama za utawala wa Safavi nchini Iran, wazungu wakitumia mbinu mbalimbali kama kuleta nguvukazi, utalii, biashara na hata timu za madaktari walikuweko nchini Iran lengo lao likiwa ni kueneza Ukristo. Historia inaonyesha kuwa, madola ya Ulaya yalikuwa yakiwatuma watu maalumu nchini Iran kwa ajili ya kubadilisha dini ya wananchi hawa na wahusika waliokuwa na jukumu hilo walikuwa wakifanya njama za kuzusha utata kupitia kuchapisha na kusambaza vitabu au vikao vya mahubiri ya kipropaganda ili kuonyesha itikadi ya Uislamu mbele ya macho ya watu kwamba, siyo sahihi.

Katika mazingira kama haya, jukumu muhimu zaidi la Maulamaa wa Kiislamu lilikuwa ni kutetea kimantiki na kiakili nguzo na misingi ya dini.  Utetezi na ubainishaji wa itikadi za dini ya Uislamu kabla ya hapo pia ulikuwa ukifanywa na Maulamaa katika fremu ya Elimu ya Teolojia. Elimu ya Teolojia ilikuwa ikitumia vyanzo viwili  kwa pamoja ambavyo ni akili na nakili na ilikuwa na mbinu yake mahususi. Lakini pindi wanafalsafa wa Kishia walipotambua kwamba, mbinu ya Kifalsafa ni bora kuliko mbinu ya teolojia na inaweza kutoa majibu ya shubha zilizopo na kulinda nguzo na misingi ya dini, waliamua kutanguliza mbinu hii.

Miongoni mwa wanafalsafa wa Kiislamu walikiweko kama akina Farabi, Ibn Sina, Ibn Rush, Khaje Nasir al-Din al-Tusi, Shahab ad-Din Suhrawardi, Mir Damad na Mullah Sadra ambao walikuwa na mtindo na mfumo maalumu wa Kifalsafa. Baina yao, mifumo wa Kifalsafa ya Ibn Sina, Mir Damad na Mulla Sadra ina mshabaha mkubwa. Inaelezwa kuwa, Ibn Sina alianza harakati hiyo, Mir Damad akaiendeleza na Mulla Sadra akaikamilisha. Kila mmoja kati ya hawa alileta kitu muhimu katika mwenendo wa fikra za Kiislamu.

 

Ibn Sina alikuwa mfuasi mkubwa wa Aristotle pamoja na mtindo wa falsafa yake uliojulikana kama Falsafah al-Masha'I {Peripatetic School}. Aristotle, alikuwa mwanafalsafa mkubwa wa maktaba ya Kigiriki. Alikuwa akiamini kwamba, ili kutoa majibu ya maswali haya ya kimsingi, inatosha tu mtu kutumia akili yake kwa njia sahihi. Aristotle alifanya juhudi za kuandaa kanuni za kufikiri kwa njia sahihi {mantiki} ili kuwazuia wanadamu kukosea katika fikra ili kwa njia hiyo nuru ya akili iweze kuangazia ukweli na uhakika wa mambo. Abu Ali Sina anayejulika katika ulimwengu wa Magharibi kama Avicenna alikuwa akifungamana kikamilifu na misingi ya falsafa ya Aristotle, lakini alikuwa akiamini kuwa, akili na dini havina mkinzano na kwamba, kila ambacho akili itahukumu basi dini pia inakikubali na kwa upande mwingine, endapo sheria zote za dini zitafahamika vyema basi hili litaungwa mkono na akili. Hivyo alichofanya Ibn Sina ni kujaribu kutabikisha falsafa ya Aristotle na misingi pamoja na itikadi za dini. Lakini pamoja na jitihada zote hizo zilizofanywa na Ibn Sina kwa ajili ya kuleta uratibu baina ya falsafa na dini, kwa uoni na mtazano wa wakosoaji, ni kwamba, hakuweza kupata mafanikio ya kuzingatiwa.

Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad alikuwa akiamini kwamba, Ibn Sina na Suhrawardi; licha ya kuwa walifanya juhudi za kuthaminiwa, lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyefanikiwa kutabikisha mfumo wake wa falsafa na  dini ya Uislamu na Madhehebu ya Kishia. Sababu ya hilo ilitokana na wao kutokuwa na ubobezi wa kutosha katika vyanzo vya dini na mbinu yao ya kutabikisha akili na sheria. Lakini kwa upande wake Mir Damad yeye kwa miaka mingi alisoma kwa wanazuoni na wasomi wakubwa wa hadithi na roho yake ilikuwa na upepo mwanana wa maneno na hadithi za Maasumina {a.s}. Mwanafalsafa huyu akiwa angali kijana mdogo, alikuwa na idhini na ruhusa kutoka kwa Maulamaa watajika wa zama hizo ya kunakili hadithi na alikuwa amebobea na kuwa na ufahamu kamili wa vyanzo muhimu vya hadithi vya Mashia. Aidha Mir Damad alikuwa na kipaji na umahiri usio na mithili katika elimu ya tafsiri na taawili ya Aya za Qur’ani Tukufu. Sifa hizi zilimfanya Mir Damad apate mafanikio makubwa ikilinganishwa na wanazuoni waliomtangulia katika kutabikisha dini na falsafa.

Kimsingi Mir Damad ndiye muasisi wa maktaba ya falsafa ya Isfahan.  Wanazuoni na wasomi waliokulia na kuondokea katika maktaba hiyo ya kifikra, mbali na kubobea na kutabahari katika Qur’ani na tafsiri yake, walikuwa na ufahamu kamili kuhusiana na hadithi za Maasumina {a.s}. Historia inaonyesha kuwa, Mir Damad alikuwa na mchango mkubwa katika kuweka jiwe la msingi la falsafa ya Kishia iliyojengeka juu ya msingi wa hadithi na maarifa ya Kiislamu.

Mwaka 1040 Hijria Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad akiwa amefunga safari kwa ajili ya kwenda kuzuru Haram za Maimamu Maasumina huko Karbala na Najaf Iraq, aliugua sana. Akiwa na umri wa miaka 70, maradhi hayo yalimsumbua sana na akaaga dunia jirani na mji wa Najaf. Mwili wake ulipelekewa kwa taadhima na heshima zote katika mji wa Najaf na kuzikwa kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib. Kwa msingi huo, daftari la maisha ya mwanafalsafa huyu mkubwa katika Ulimwengu  wa Kiislamu likawa limefungwa na kuacha nyuma historia inayong’ara na iolyojaa fahari kubwa ya mafunzo ya dini na mitazamo yake kuhusiana na falsafa.

Wapenzi wasikilizaji, muda wetu kwa leo umefikia tamati hivyo sina budi kukuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh