Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (34)
Ahlan Wasahlan wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.
Vipindi vyetu viwili vilivyopita vilitupia jicho kwa mukhtasari maisha ya alimu na msomi mashuhuri wa Kishia yaani Mir Mohammad Baqer Asterabadi, mashuhuri zaidi kwa jina la Mir Damad mmoja wa wanafalsafa mahiri wa Kishia. Tulisema kuwa, Mir Mohammad ni mwanafalsafa mkubwa, mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mshairi mahiri wa Kishia. Tuliona jinsi msomi huyu alivyokuwa na mchango mkubwa katika uga wa falsafa hasa katika zama ambazo ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kutoka kwa ustaarabu wa Magharibi. Sehemu ya 34 ya mfululizo huu juma hili itamzungumza Sadruddin Muhamammad bin Ibrahim Shirazi mashuhuri zaidi kwa jina la Mulla Sadra, mwanafalsafa mkubwa kabisa katika Ulimwengu wa Kiislamu. Jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi.
Sadruddin Muhamammad bin Ibrahim Shirazi mashuhuri zaidi kwa jina la Mulla Sadra ni mwanafalsafa, arif na mfasiri mkubwa wa Qur'ani wa Kishia wa karne ya 10 na 11 Hijria. Msomi huyu anayejulikana pia kama Sadr al-Mutaalihin ndiye muasisi wa Maktaba ya Kifalsafa ya Hikmatul-MutaaliyaH inayojulikana kama maktaba ya tatu muhimu ya Kifalsafa katika Ulimwengu wa Kiislamu. Mulla Sadra alizaliwa mwaka 979 kwa kalenda ya Kiislamu katika mji wa Shiraz moja ya miji ya Iran. Shiraz ni mji ambao unasifika kwa kuchomoza na kuchipukia wasomi na wanazuoni wengi wakubwa nchini Iran.

Baba yake alikuwa mtu mtajika ambaye licha ya kuwa na utajiri na uwezo mkubwa, hakuwa na mtoto. Alimuomba Mwenyezi Mungu na kutia nia kwamba, kama Allah atamjaalia na kumruzuku mtoto basi atatenga sehemu ya utajiri wake kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa sambamba na kuwasaidia masikini. Mwenyezi Mungu akamjibu dua yake baada ya kumjaalia mtoto ambaye alimpa jina la Muhammad. Muhammad ambaye ndiye Mulla Sadra tunayemzungumzia leo, alianza kusoma masomo yake ya awali nyumbani kwa baba chini ya walimu mahususi ambapo mwanzoni tu mwa masomo yake kipaji na maarifa ya hali ya juu aliyokuwa nayo yalidhihiri na kujitokeza kwa walimu wake ambao walikiri wazi hilo.
Baada ya kukamilisha masomo ya awali alielekea katika mji wa Qazvin akiwa pamoja na familia yake. Katika zama hizo, mji wa Qazvin ulikuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi na kituo kikuu cha elimu na maarifa ambapo Maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Sheikh Bahai na Mir Damad walikuwa wakifundisha katika mji huo. Akiwa katika mji huo, Sadruddin Muhamammad aliendelea na masomo kwa walimu hao na kufanikiwa kufikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi.
Mulla Sadra akiwa mwalimu kamili na asiye na mithili alianza kujishughulisha na kazi ya kufundisha katika shule mbalimbali za Isafahan. Baada ya muda aliandamwa na Maulamaa wengine na kutuhumiwa kwamba, ni mzushi na mtu wa bidaa katika dini. Lililomponza ni mitazamo yake Kifikihi na Kifalsafa ambayo ilitofautiana na wanazuoni na wasomi wengine wa zama hizo.
Baada ya kuona kuwa, katika mazingira haya hana fursa ya kubainisha masuala mbalimbali ya kielimu katika mji huo, alifunga safari na kuelekea katika mji wa Qum. Akiwa katika mji huo pia, Mulla Sadra alikabiliwa na changamoto kubwa baada ya kutengwa na Maulamaa wa mji huo. Hata hivyo hakuondoka katika mji huo na badala yake alichagua moja ya vijiji vya mji huo na kujitenga. Historia inaonyesha kuwa, Mulla Sadra aliishi katika kijiji alichokichagua cha Kohak kwa muda wa miaka 7 huku baadhi ya riwaya zikisema miaka 15. Ala kulli haal, kutokana na maudhi aliyokuwa ameyapata alijiweka mbali na masuala ya kufundisha na kualifu vitabu. Maisha ya upweke ya Mulla Sadra, yakawa fursa mwafaka kwake ya kujijenga kinafsi na kukata masafa kuelekea katika saada na ukamilifu. Katika kipindi hiki, Mulla Sadra alijihusisha na kufanya ibada na jihadi ya nafsi.
Baada ya kumalizika kipindi cha kujitenga, ilianza duru ya tatu ya maisha ya Mulla Sadra au Sadr al-Mutaalihin kama anavyojulikana pia. Kipindi hiki kilianza kwa Mulla Sadra kushika kalamu na kuanza kuandika vitabu na kuibuka na kitabu cha Al-Hikmat al-Muta'aliyyah Fi al-Asfar al-Arba'ah athari na kitabu muhimu zaidi cha mwanafalsafa huyo. Katika kitabu hiki, Mulla Sadra amearifisha na kutambulisha mfumo mpya wa Kifalsafa ambao uliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Al-Hikmat al-Muta'aliyyah, na kuanzia wakati huo mpaka leo, mfumo huu umekuwa na wafuasi wengi zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika mfumo wake huu, anabainisha na kuelezea masuala mbalimbali ya Kifalsafa kwa kutumia mbinu za kiakili, nakili, ushuhuda wa Kiirfani na kadhalika.
Ilikuwa takribani mwaka 1040 Hijria, wakati Mulla Sadra aliporejea katika mji aliozaliwa wa Shiraz. Inaelezwa kuwa, mtawala wa wakati huo alimualika Shiraz ilia akasimamie shule moja. Akiwa Shiraz pia, Mulla Sadra alifundisha falsafa, tafsiri ya Qur'ani na hadithi na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi.
Mulla Sadra amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa. Inaelezwa kuwa, kuna athari zaidi ya 50 za maandishi ambapo kitabu muhimu zaidi ni cha Al-Hikmat al-Muta'aliyyah Fi al-Asfar al-Arba'ah. Mbali na vitabu vyake vya Falsafa, Mulla Sadra ana vitabu vingine pia katika uga wa Tafsiri ya Qur'ani na Usul Kafi. Aidha watoto wake sita kila mmoja aliondokea kuwa alimu na msomi mkubwa.

Katika kipindi cha umri wake wa miaka 71 Mulla Sadra alifanya safari mara saba kwa miguu kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Hii ni katika hali ambayo, katika zama hizo safari ndefu ya kutembea kwa miguu kuelekea Makka kwa ajili ya kufanya ibada ya Hija ilikuwa na mashaka na taabu nyingi njiani. Hata hivyo hilo halikumzuia Mulla Sadra kusafiri mara saba kwa miguu kwenda Hija akitekeleza maagizo na sunna ya shakhsia wakubwa katika dini. Safari yake ya saba aliifanya akiwa na umri wa miaka 71 na ni katika safari hiyo ambapo maisha yake yalifikia tamati. Mwili wa Mulla Sadra ulipelekwa katika mji wa Najaf nchini Iraq na kuzikwa kando ya Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib {a.s}.
Wapenzi wasikiliza muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati kwa leo. Hata hivyo kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, kama ambavyo kumalizika kwa muda wa kipindi hiki ndio mwanzo wa kuanza harakati za kuandaa sehemu nyingine ya kipindi hiki kwa ajili yenu juma lijalo. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.