Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (35)
Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki.
Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichotangulia kilimzungumzia Sadruddin Muhamammad bin Ibrahim Shirazi mashuhuri zaidi kwa jina la Mulla Sadra. Tulisema kuwa, Mulla Sadra ndiye muasisi wa Maktaba ya Kifalsafa ya Hikmatul-Mutaaliya inayojulikana kama maktaba ya tatu muhimu ya Kifalsafa katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tuliona jinsi Mulla Sadr alivyokabailiwa na changamoto mbalimbali maishani ikiwemo ya kutengwa kutokana na mitazamo yake ya kielimu ambayo ilitofautiana na ya wasomi na wanazuoni wa zama zake. Sehemu ya 35 ya kipindi hiki juma hili itamzungumzia Allama Faydh Kashani, msomi mwingine mtajika wa Kishia aliyekuwa amebobea katika elimu za falsafa, tafsiri na utambuzi wa hadithi katika karne ya 11 Hijria. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mulla Muhsin Faydh Kashani alizaliwa mwaka 1007 Hijria katika mji wa kihistoria na kiutamaduni wa Kashan moja ya miji mikongwe ya Iran. Baba yake ambaye ni Radhiuddin Shah Murtadha alikuwa msomi aliondokea kuwa mashuhuri kama fakihi, mwanateolojia, mfasiri wa Qur'ani na mawanafasihi mashuhuri wa mji wa Kashan; na mama yake Zahra Khatun alikuwa mwanamke msomi, mshairi na ni binti wa Dhiyaaul Urafaa Razi, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa mji wa Shahr-e-Rey nchini Iran. Muhsin alibakia na baba yake kwa miaka miwili tu, kwani baadaye alichukuliwa na mjomba wake ambaye alichukuua jukumu la kumlea na kumfundisha masomo ya msingi ya kidini.
Katika zama hizo, mji wa Isafahan ulikuwa mji mkuu wa Iran na kituo cha kujumuika Maulamaa na walimu mahiri na stadi katika taaluma mbali mbali za Kiislamu. Sheikh Bahai, Mulla Sadra na Mir Damad ambao tuliwazungumzia katika vipindi vyetu vilivyotangulia walikuwa wameugeuza mji huo na kuufanya kuwa kambi ya kielimu ya Ulimwengu wa Kiislamu. Mulla Muhsin au Faydh Kashani kama anavyojulikana zaidi, aliweza kuitumia vizuri fursa hiyo kadiri alivyoweza na kunufaika na bahari hiyo ya elimu ya wasomi na wanazuoni hao.
Allama Faydh Kashani akiwa na hima na idili kubwa katika kusoma na kutafuta elimu, aliweza kukwea daraja za kielimu moja baada ya nyingine na kufanikiwa kupata idhini ya kunukuu hadithi kutoka kwa Sheikh Bahai. Idhini hiyo ilikuwa na maana kwamba, mwanafunzi huyo amefikia hatua na marhala ya utambuzi wa hadithi na hivyo kuanzia hapo ana idhini ya kunukuu hadithi na kuelezea mtazamo wake kuhusiana na kiwango cha ukweli wa hadithi na kadhalika. Baada ya hapo Faydh Kashani alianza kufanya safari katika miji mingine ili aweze kustafidi na elimu za wasomi wengine wa miji hiyo. Faydh Kashani alifanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad akiwa katika rika la ujana na akawa mwenye nadharia na mitazamo katika masuala mbalimbali ya fikihi huku mafakihi na wanazuoni wakubwa wa elimu hiyo wakiunga mkono na kuthibitisha Ijtihad yake.
Faydh Kashani alikuwa msomi mwenye hima na idili ya hali ya juu aliyekuwa amebobea katika taaluma na elimu tofauti. Msomi huyo ana vitabu vingi alivyoalifu katika nyanja mbalimbali. Alianza kazi ya utunzi na kualifu vitabu akiwa na umri wa miaka 17 na katika kipindi cha umri wake wa miaka 65 aliandika vitabu karibu 140 ambapo kila kimoja kati ya vitabu hivyo kilikuwa na mchango na taathira ya kuzingatiwa katika kuinua utamaduni na elimu ya jamii ya Kiislamu.
Moja ya athari hizo ni Tafsiri al-Safi, moja ya tafsiri za Qur'ani zenye itibari. Akiwa na lengo la kuandika tafsiri hii, Allama Kashani alizisoma kwa umakini tafsiri nyingine za Qur'ani zilizokuwa zimeandikwa na Maulamaa wa Kishia na Kisuni na kisha ndipo akaandika Tafsir al-Safi kwa msingi wa hadithi na riwaya pamoja na nyaraka za Kishia.
Kitabu kingine cha Allama Faydh Kashani ni al-Wafi ambacho kinahusiana na hadithi. Akiwa na nia ya kuandika kitabu cha al-Wafi, Faydh Kashani alivisoma vitabu vya Kutubul-Arbaa vya Mashia yaani Kafi, Tahdhib, Istibsaar na Man la Yahdhuruh al-Faqih. Faydh Kashani ana vitabu vingine pia katika uga wa teolojia, Irfan, Akhlaq na fasihi.
Licha ya kuwa, Allama Faydh Kashani alikuwa Mujtahidi mwenye uwezo na mwalimu mahiri lakini bado alikuwa na kiu ya kusoma na kuongeza maarifa. Alimu huyu alikuwa na hali ya kutotosheka na elimu, na elimu aliyokuwa nayo alikuwa akiaminui kwamba, haimtoshi kwa ajili ya kufikia katika ukamilifu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Faydh Kashani alikuwa akiipa umuhimu maalumu Swala ya Ijumaa na alikuwa akiamini kwamba, Swala hiyo ni wajibu kwa Waislamu katika kipindi cha Ghaiba ya Maasumu (a.s), na mtu ambaye anatekeleza ibada hiyo ya Swala ya Ijumaa siyo wajibu kwake kuswali Swala ya Adhuhuri, yaani Swala ya Ijumaa inatosheleza hivyo hakuna haja ya kuswali Swala ya Adhuhuri.
Allama Faydh Kashani alifahamika pia kwa sifa njema za kimaadili. Alikuwa mpole na mwenye kuamiliana na watu kwa maadili na mwenendo bora kabisa. Mwanazuoni huyo alikuwa akimzingatia mno Imam wa Zama Imam Mahdi (atfs). Kitabu cha Shauq Mahdi ni athari iliyoachwa na Faydh Kashani. Katika utangulizi wa kitabu hicho Faydh Kashani ameeleza huba, shauku na mapenzi yake makubwa aliyonayo kwa Imam Mahdi na Maimamu wengine watoharifu (a.s).
Kwa upande wa familia yake, Faydh Kashani alikuwa na watoto 6, mabinti watatu na watoto wa kiume watatu, ambapo watoto wote hawa wa kiume waliondokea kuwa wasomi na wanazuoni watajika katika zama zao. Allama Muhammad Alamul-Huda, mwana mkubwa wa Faydh Kashani ni fakihi na muhaddith mkubwa. Watoto wake wengine wawili wa kiume yaani Nurul-Huda na Muinuddin nao walikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa katika zama zao.
Mulla Muhsin Faydh Kashani aliaga dunia huko Kashan akiwa na umri wa miaka 84 na kuzikwa katika mji huo huo aliozaliwa. Kutokana na tawadhui na unyenyekevu aliokuwa nao aliusia kaburi lake lisijengewe kivuli. Hii leo licha ya kupita miaka zaidi ya miaka 300, kaburi lake lingali ziara na sehemu ya kutembelewa na watu wanaoonyesha heshima yao kwa alimu na msomi huyo mahiri. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amfufue pamoja na Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh