Jumapili tarehe 5 Disemba 2021
Leo ni Jumapili tarehe 29 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2021.
Miaka 770 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu la Shamsuddin, mpokeaji wa Hadithi za Mtume (saw) na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya Hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa Hadithi nyingi sana kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Dhahabi alifuatilia matukio ya historia ya Uislamu na watu mashuhuri ya kuanzia wakati wa kudhihiri Uislamu hadi mwaka 704 na kuandika habari na matukuio ya wataalamu wa hadithi wa zama hizo. Matukio hayo aliyakusanya katika kitabu alichokipa jina la Historia ya Uislamu. Vitabu vingine vya msomi huyo ni pamoja na Tabaqatul Qurraa, al Muujamul Saghiir na al Muujamul Kabiir.
Miaka 186 iliyopita katika siku kama ya leo, Mirza Abul-Qassim Qaim Maqam Farahani mmoja wa waandishi na wanasiasa wa Iran aliauawa katika kipindi cha utawala wa Qajar. Aliteuliwa kuwa kaimu wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Qajar na baadaye kuchaguliwa kuwa Kansela wa Muhammad Shah. Qaim Maqam Farahani alifanya huduma na kuchukua hatua nyingi za marekebisho nchini Iran. Hata hivyo wasiomtakia mema wa ndani ya Iran na wakoloni wa nje ambao hawakufarahishwa na mambo aliyokuwa akiyafanya yaliyokuwa yakipingana na maslahi yao haramu waliandaa uwanja wa kumuua mwanasiasa huyo.
Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar. Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.
Tarehe 5 Disemba miaka 128 iliyopita alizaliwa Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni mwa kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Nelson Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Baada ya kushika hatamu za uongozi, Mandela aliamiliana vyema na watala wa zamani wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na hata wale waliomfunga jela na kumtesa. Mwenendo huo wa kusamehe ulizidisha umashuhuri na kupendwa shujaa huyo, na mwaka 1993 alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel. Kitabu mashuhuri zaidi cha shujaa huyo wa Afrika ni kile chenye kumbukumbu zake alichokipa jina la: "Njia Ndefu ya Kuelekea kwenye Uhuru".
Na Leo tarehe 5 Desemba ni Siku ya Kimataifa ya Watu Wanaojitolea katika Nyanja za Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii. Kutenda wema na kufanya hisani ni suala ambalo halihusu, dini, taifa, wala kaumu makhsusi. Hata hivyo Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, umehimiza zaidi kutenda wema na hisani na kuwataja wahisani na watenda wema kwamba ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 195 ya Suratul Baqara inasema: Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wahisani.