Feb 11, 2022 02:35 UTC
  • Ijumaa tarehe 11 Februari 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 9 Rajab 1443 Hijria sawa na Februari 11 mwaka 2022.

Tarehe 22 Bahman miaka 43 iliyopita Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme. Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote. Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita sawa na tarehe 11 Februari 1990, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa miaka 27. Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Lakini baada ya miaka kadhaa aliachiliwa huru kutokana na msimamo wake thabiti akiwa jela, mapambano ya wananchi wa nchi hiyo pamoja na mashinikizo yaliyotokana na fikra za waliowengi duniani.

Mzee Nelson Mandela

Katika siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, Dikteta Hosni Mubaraka wa Misri ambaye alijitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo aling'olewa madarakani kufuatia harakati za mapinduzi za wananchi. Hosni Mubarak ambaye alikuwa Makamu wa Rais Anwar Sadat wa Misri aliingia madarakani mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi huyo. Anwar Sadat aliuawa na Khalid Islambuli afisa wa jeshi la Misri baada ya kusaini makubaliano ya Camp David na Israel. Mubarak naye baada ya kuingia madarakani aliendeleza mwenendo huo huo wa kuwatetea Wazayuni na kutekeleza siasa za Marekani na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati. Ndani ya nchi pia Mubarak sambamba na kutangaza hali ya hatari ya muda mrefu alitekeleza siasa za kuwakandamiza wananchi hasa wanaharakati wa Kiislamu. Hayo na mengine mengi hatimaye yalipelekea Misri kuwa nchi ya kwanza kuathiriwa na vuguvugu la mwamko wa Kiislamu na wimbi la kukabiliana na udikteta lililoanzia nchini Tunisia na kuanguka utawala wa muda mrefu wa dikteta huyo wa Misri katika siku kama ya leo.

René Descartes

Siku kama ya leo miaka 372 iliyopita alifariki dunia René Descartes, mwanafalsafa na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Alizaliwa tarehe 31 Machi 1596 Miladia na baada ya masomo yake ya msingi alianza kusomea hisabati na tiba. Baadaye Descartes alibobea katika fani ya hisabati na uhandisi huku muda mfupi baadaye akianzisha utafiti pia katika uga wa falsafa. Aidha msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika fani nyinginezo za kielimu. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

René Descartes

Miaka 2682 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme duniani ambao ungali unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye anayeendesha masuala ya nchi.

 

Tags