Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (39)
Assalaam alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya kutoka hapa mjini Tehran.
Karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, bila kusahau athari na vitabu vyao. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Muhammad Taqi Majlisi, baba wa Allama Majlisi, mmoja wa Maulamaa wakubwa na watajika wa Kishia katika karne ya 11 Hijria.
Tulisema kuwa, msomi huyu alizaliwa katika mji mkubwa na mzuri wa Isafahan uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi nchini Iran wakati huo. Aidha tulieleza kuwa, baada ya Muhammad Taqi kumaliza masomo ya msingi na ya awali ya dini kwa baba yake, alianza kuhudhuria masomo ya walimu wakubwa na waliokuwa mashuhuri katika zama hizo. Kitabu mashuhuri zaidi cha Muhammad Taqi Majlisi ni Raudhat al-Mutaqin. Karibuni kutegea sikio sehemu ya 39 ambayo itatupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Muhammad Baqir bin Muhammad Taqi mashuhuri kwa jina la Allama Majlisi.
Katika moja ya masiku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka 1037 Hijria, alizaliwa mtoto katika nyumba ya Sheikh Muhammad Taqi Majlisi mujtahidi mtajika na mwanazoni mchamungu wa Kishia. Mtoto huyu alikuwa na kuifanya familia ya Majlisi kufikia katika kilele cha taqwa na uchajimungu. Baba yake alimpa mtoto huyu jina la Muhammd Baqir akitabaruku kwa jina la Imam wa tano wa Waislamu wa madhehebu ya Shia yaani Imam Muhammad Baqir (as).
Baba yake alifanya hima kubwa kumlea mtoto huyo sambamba na kumfundisha. Familia ya Majlisi kwao ni Jabal Amili nchini Lebanon lakini ilikuwa imehajiri na kuja Iran. Familia hii ilikuwa mashuhuri kwa kushikamana na madhehebu ya Ushia katika karne ya tano Hijiria na akthari ya watu wa familia hii katika karne ya 10 na 11 Hijria walikuwa wakihesabiwa kuwa wasomi, wanazuoni na Maulamaa mashuhuri.
Muhammad alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika masuala ya elimu tangu akiwa mdogo wakati huo akiwa chini ya malenzi na mafundisho ya baba yake. Baba yake alikuwa mwanazuoni msomi na mchamungu. Muhammad Baqir alisoma elimu mashuhuri za zama hizo kwa mzazi wake huyo wa kiume. Histroria inaonyesha kuwa, Allama Majlisi alichanua na nuru ya elimu yake kujitokeza tangu akiwa angali kijana na barobaro. Alipofikisha umri wa miaka 14 alipata idhini kutoka kwa Mulla Sadra mwanafalsafa mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kupokea na kunakili hadithi na riwaya.

Aliweza kuzisoma kwa muda mchache mno elimu na masomo ya Hawza wakati huo kama Nahw, Sarf, maani, balagha, bayani, lugha, hisabati, historia, falsafa, hadithi, elmur rijaa, usul, fikihi, teolojia na kadhalika na kufikia daraja ya kuwa mwalimu katika taaluma hizo. Aidha ni katika kipindi hicho pia ambapo alikuwa tayari na vitabu mbalimbali alivyoandika katika elimu tofauti.
Allama Majlisi alisoma kwa baba yake kuliko kwa mwalimu mwingine yeyote. Kutokana na kuwa, baba yake alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Bahai, Allama Majlisi naye akawa amenufaika na kuathirika na fikra pamoja na mitazamo ya Sheikh Bahai katika masuala mbalimbali ya kielimu.
Akiwa katika rika la ujana, Allama Majlisi alisoma pia kwa wasomi na wanazuoni mashuhuri kama Mulla Abdallah Shushtari, Sheikh Abdallah bin Jabir Amoli, Sheikh Ali Jabal Amili na wasomi na wanazuoni wengine wakubwa na watajika katika zama hizo hususan kwa fakihi, mwanafalsafa na mpokezi wa hadithi mtajika yaani Mulla Hassan Feydh Kashani.
Imenukuliwa katika vitabu na vyanzo vyenye itibari kisa cha baba yake Allama Majlisi. Muhammad Taqi Majlisi ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Majlisi wa Kwanza anasimuulia kwamba: Usiku mmoja nililia baada ya kuswali na kuomba dua. Ilikuwa katikati ya siku. Nikapatwa hali fulani ya kuhisi kwamba, dua yangu itajibiwa. Nikawa nafikiria na kujiuliza katika lahadha hii niombe nini kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Je niombe haja ya kidunia au ya akhera? Ghafla nikasikia sauti ya mwanangu yaani Muhammad Baqir akilia akiwa katika susu. Nikanyayua mikono kwa ajili ya dua na kusema: Ewe Mola wangu! Nakuomba kwa haki ya Muhammad na aali zake watoharifu, mjaalie mtoto huyu aje kuwa muenezaji wa dini na msambazaji wa sheria za Sayyid al-Mursalin Muhammad bin Abdillah na umjaalie na kumpa tawfiki isiyo na kikomo." Kwa hakika hii ni dua ambayo ilikubaliwa kwa ajili ya mtoto huyu ambaye baadaye aliondokea kuwa msomi na mwanazuoni aliyetumia umri wake kuhudumia Uislamu na mafundisho yake.
Moja ya huduma kubwa na yenye thamani mno ya Allama Majlisi na ambayo inahesabiwa kuwa dafina na hazina isiyo na mithili ni hatua yake ya kukukusanya na kuandika hadithi katika kitabu cha mijalada mingi. Akthari ya vitabu vya hadithi vilikuwa vimepotea kutokana na vita na machafuko katika mataifa ya Kiislamu.
Allama Majlisi kutokana na kufahamu na kudiriki udharura na haja kubwa ya vitabu vya hadithi, alifanya hima na idili kubwa na kuandika kitabu cha hadithi cha Bihar al-Anwar. Mwanazuoni huyu akiwa na lengo la kulinda utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu alilalizimika kusimama na kukabiliana na wapinzani na maadui wa Uislamu na Ushia.
Miongoni mwa kazi nyingine zilizofanywa na alimu na msomi huyu kwa ajili ya kulinda vyanzo vya hadithi na riwaya za Waislamuu wa Kishia ni kuwashajiisha wanafunzi wa masomo ya dini kusoma na kufanya uhakiki wa hadithi, kwani wanafunzi walikuwa wamejitenga kabisa na hadithi kwa muda mrefu. Aidha alitangaza kuwa, kila mwanafunzi ambaye ataweza kuandika nakala moja miongoni mwa Kutub al-Arabaa yaani vitabu vinne vya Waislamu wa Kishia vinavyohusiana na hadithi na ikawa haina makosa, basi atapata ijaza na idhini kutoka kwake ya kunukuu hadithi.
Hapana shaka kuwa, huduma kubwa iliyofanywa na Allama Majlisi katika ulimwengu wa Kiislamu ni kubwa mno na haiwezekani kuyaeleza yote hayo katika kipindi kimoja. Hivyo basi msisite kujiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu ambapo tutaendelea kumzungumzia alimu msomi huyo pamoja na athari zake.
Hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh