Mar 07, 2022 23:21 UTC
  • Jumanne tarehe 8 Machi 2022

Leo ni Jumanne tarehe 5 Shaabani 1443 Hijria sawa na tarehe 8 Machi mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Miaka 1130 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.

Muhammad bin Zakaria Razi

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Dikteta Ferdinand Marcos

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon. 

Leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.