Jumapili, 13 Machi, 2022
Leo ni Jumapili tarehe 10 Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe 13 Machi 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1021 iliyopita, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 422 Hijria, aliaga dunia Abu Abdullah Abdulbaqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijria. Alikuwa akiishi katika mji wa Baghdad, ilipo Iraq ya sasa. Mbali na kupata elimu kwa malenga na wanafasihi wakubwa, Abdulbaqi alikuwa akihudhuria pia darsa za maulamaa watajika wa mji huo katika zama hizo na kufaidika kwa elimu mbalimbali hasa elimu ya Hadithi. Abu Abdullah Abdulbaqi alikuwa na kipaji cha maumbile cha kusanifu mashairi na ameacha athari nyingi katika uga huo. ***

Miaka 689 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 754 Hijria aliaga dunia Majdu-ddin Abul Fawaaris, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq; na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alikamilisha masomo yake ya dini kwa maulamaa wakubwa, mpaka yeye mwenyewe akafikia daraja ya kuwa alimu mwenye wanafunzi walio chini yake. Alichota elimu nyingi katika fani za Fiqhi, Usul-Fiqhi, Hadithi, Ilmul-Kalam, Tafsiri ya Qur'ani na Fasihi ya Kiarabu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameacha athari nyingi, miongoni mwazo ni kitabu kiitwacho Kanzul-Fawaaid. ***
Siku kama ya leo miaka 289 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia na elimu hiyo ilikuwa imepiga hatua. Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea na gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804. ***
Miaka 74 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo. ***

Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Esfand 1358 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini MA alitoa amri ya kuundwa taasisi ambayo itakuwa ikishughulikia hali za familia za mashahidi waliouawa wakitetea Mapinduzi ya Kiislamu nchini. Taasisi hiyo hadi sasa bado inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi kwa familia za mashahidi wa harakati za mapinduzi na hali kadhalika familia za mashahidi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. ***
