Mar 29, 2022 21:48 UTC
  • Jumatano, Machi 30, 2022

Leo ni Jumatano tarehe 27 Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe 30 Machi mwaka 2022 Milaadia.

Miaka 177 iliyopita katika siku kama ya leo aliuawa Sayyid Ali Muhammad Shirazi aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya “Bab” ambaye alidai kuwa ndiye Imam Mahdi (AF) na baadaye akadai kuwa ni Mtume. Alizaliwa mwaka 1235 Hijria Qamariya katika mji wa Shiraz nchini Iran na alionekana kuwa na itikadi potofu akiwa bado shuleni. Muhammad Ali Bab ambaye hakuwa na elimu ya juu alifuatwa na watu majahili na kuungwa mkono na wakoloni. Baada ya kudai kuwa ndiye Imam wa mwisho katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) yaani Imam Mahdi (AF), Bab alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba dini ya Uislamu imefutwa. Wanazuoni wa zama hizo walifichua urongo wake na kuchukulia hatua. Hata hivyo aliendelea kulingania itikadi zake potofu na katika siku kama ya leo Amir Kabiir aliyekuwa kiongozi wa zama za Qajar alitoa amri ya kunyongwa kwake.

Sayyid Ali Muhammad Shirazi

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, Russia iliiuzia Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ina ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja na nusu ni jimbo la 49 la Marekani. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, hususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki.

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.

Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi

Tarehe 30 Machi miaka 46 iliyopita, maandamano makubwa yaliyopewa jina la "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, tarehe 18 Oktoba mwaka 1975, mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulianza kufanyika kura ya maoni ya nchi nzima kwa lengo la kuainisha mfumo utakaotawala hapa nchini. Kura hiyo ya maoni ya kihistoria ilifanyika kwa muda wa siku mbili kutokana na kupokelewa kwa wingi na wananchi wa Iran. Asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran, walipiga kura ya kutaka mfumo wa Kiislamu utawale hapa nchini.