Mar 30, 2022 22:00 UTC
  • Alkhamisi tarehe 31 Machi mwaka 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Shaaban 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 31 Machi mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 813 iliyopita alifariki dunia Ibn Hajib, mtaalamu wa Hadithi na mwanahistoria maarufu wa Kiislamu. Ibn Hajib alizaliwa mwaka 593 Hijiria huko Damascus, Syria na kuelekea kwenye miji tofauti kwa ajili ya kusomea elimu ya Hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa wakati huo. Alitambuliwa kuwa gwiji wa elimu ya Hadithi katika zama zake kutokana na umahiri wake mkubwa katika taaluma hiyo. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa.

Ibn Hajib

Miaka 426 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

Rene Descartes

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.

Anwar Sadat