Mar 31, 2022 22:06 UTC
  • Ijumaa, Aprili 1, 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe Mosi Aprili mwaka 2022 milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1218 iliyopita alifariki dunia Fadhlu Bin Dukain maarufu kwa jina la Ibn Nuaim, mtaalamu wa Hadithi, fiq'hi na mwanahistoria. Ibn Nuaim aliyezaliwa mwaka 130 Hijiria nchini Iraq, alikuwa mmoja wa wapokezi mashuhuri wa Hadithi aliyepewa heshima na maulama wakubwa wa Kiislamu wa zama hizo. Kitabu cha "al Swalat' ni miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1125 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mtaalamu wa Hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza elimu ya fiq'hi na Hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake. Baadaye alielekea Makkah, ambapo alijifunza elimu ya Hadithi hadi mwisho wa uhai wake. Akiwa Makkah Ibn Mindhir alijishughulisha na uandishi wa vitabu. Katika kitabu cha 'Al-Ijmaa' alibainisha na kufafanua nadharia tofauti za wasomi katika uwanja wa sheria za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Ashraf kinachoonesha umahiri wake mkubwa katika taaluma ya Hadithi.

Miaka 444 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.

William Harvey

Tarehe Mosi Aprili miaka 77 iliyopita vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege elfu 10 za kivita za Marekani zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa siku 83. Hata hivyo Wajapani walipambana ipasavyo katika vita hivyo kwa ajili ya kulinda nchi yao kwa kadiri kwamba meli 36 za kivita za Marekani ziliharibiwa kikamilifu na nyingine 369 kutiwa hasara. Vilevile ndege za kivita 763 za Marekani zilitunguliwa. Wajapan pia walipata hasara kubwa katika vita hivyo kwani wapiganaji laki moja na elfu kumi kati ya wapiganaji wote laki moja na elfu ishirini wa kisiwa cha Okinawa waliuawa au kujeruhiwa.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi, faqihi, mfasiri wa Qur'an Tukufu na hatibu mkubwa wa Iran. Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi alizaliwa mwaka 1309 Hijiria, mjini Qum na katika familia ya elimu na maarifa ya dini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alijiunga na masomo ya hawza kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kabir Qumi, Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi, huku akisoma pia elimu ya falsafa na theolojia kwa Ayatullah Mirza Ali Akbar Mudares Yazdi ambapo alifanikiwa kufikia ngazi ya juu ya kielimu. Alikuwa miongoni mwa shakhsia waliochangia katika uhamisho wa Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kutoka mjini Arak kwenda mjini Qum na hatimaye kuasisiwa hawza ya kielimu mjini hapo. Mbali na kubobea katika utafiti na kujibu shubuha mbalimbali za dini nyingine, alikuwa mjuzi katika masuala ya historia na jografia ya dini mbalimbali ambapo alitoa nadharia katika uwanja huo. Aidha maulama mbalimbali na maraaji walikuwa wakiheshimu nadharia zake hususan katika uga wa fiqhi huku Imamu Khomein (MA) akimpa lakabu ya 'Sheikh al-Twaifa'. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Risaalatu al-Dharar' 'Mantwiqul Hussein' na 'Maqswadul-Hussein.'

Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi

Tarehe 12 Farvardin miaka 43 iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kushiriki kwa wingi wananchi katika kura ya maoni, taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kihistoria wa kupasisha mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini. Zaidi ya asilimia 98 ya walioshiriki waliupigia kura ya ndiyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tarehe 12 Farvardin kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jamhuri ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, alifariki dunia Bi. Nusrat Amin, mwanamke wa kwanza aliyefikia daraja la mujtahid katika ulimwengu wa Kiislamu. Bi. Nusrat Amin alizaliwa Isfahan, Iran mnamo mwaka 1308 Hijiria. Akiwa na umri wa miaka minne alianza kwenda katika maktaba na kujifundisha Qur'ani Tukufu na lugha ya Kifarsi. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu na kufanikiwa kufasiri kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika juzuu 15 na kuandika vitabu vingine vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni Assair Wassuluuk, Arbain al Hashimiyyah na Nafahaat Rahmaniyya.

Bi. Nusrat Amin