Jumatano, Aprili 6, 2022
Leo ni Jumatano tarehe 4 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 6 mwaka 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 867 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jina la Ibn Khurasani, mtaalamu wa lugha, malenga na mwandishi wa Baghdad. Ibn Khurasani alizaliwa mwaka 494 Hijria huko Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo baadaye alielekea Baghdad, Iraq na kuishi katika mji huo. Muhammad bin Muhammad alihitimu masomo kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Ibn Khurasan ameandika mashairi mengi ambayo mengi kati ya hayo yamepotea.

Miaka 442 iliyopita na katika siku kama ya leo, ardhi ya Ureno moja kati ya nchi zilizokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16, iliunganishwa na Uhispania. Ureno ilikuwa ikihesabiwa kama mpinzani mkuu wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo pole pole Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile kufuatia hali mbaya ya kiuchumi. Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani na ikaingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa maslahi ya Waitifaki. Kabla ya hatua hiyo, Marekani ilikuwa imekata uhusiano wake wa kisiasa na Ujerumani na ilikuwa ikizisaidia nchi Waitifaki.
Miaka 37 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ja'far Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani.
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, vita vya umwagaji damu mkubwa baina ya makabila mawili ya Watutsi na Wahutu vilianza nchini Rwanda. Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994.