Apr 13, 2022 13:28 UTC
  • Jumatano tarehe 13 Aprili 2022

Leo ni Jumatano tarehe 11 mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka 1443 Hijria sawa na Aprili 13 2022.

Siku kama ya leo miaka 590 iliyopita, alifariki dunia mjini Cairo Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na Hadithi wa Kiislamu. Baada ya kusoma Qur'ani na masomo ya awali ya kidini, Ibrahim Karaki alianza kufanya safari katika maeneo mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Kitabu cha I'rabul-Mafsal ni miongoni mwa athari zilizoachwa na msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala Bagh nchini India. Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo. Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Mahatma Ghandhi

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja dhidi ya basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon. kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon. Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Kizayuni, viliiletea hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

wanamgambo wa Kikristo, Lebanon

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani. Ayatullah Lankarani alizaliwa katika mji wa Isfahan hapa nchini Iran na katika kipindi cha ujanani alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya kupata masomo. Akiwa huko Najaf, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani aliweza kusoma chini ya maulama wakubwa wa zama zake kama vile Dhiyaudin Iraqi, Ayatullah Mirzai Naayini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kumaliza masomo yake na kufikia daraja ya juu ya elimu alirudi katika mji alikozaliwa wa Isfahan na kutumia umri wake wote katika kutoa mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu. Ayatullah Lankarani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani

Katika siku kama hii ya lo miaka 19 iliyopita yalifanyika maandamano ya kwanza ya watu wa Iraq dhidi ya wavamizi wa nchi hiyo baada ya miongo mitatu ya ukandamizaji wa serikali ya Saddam Hussein. Baada ya kuanguka utawala wa Saddam Hussein na chama cha Baath huko Iraq mnamo Aprili 9, 2003 na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na vikosi vya wavamizi, haswa wanajeshi wa Marekani, maandamano ya kwanza makubwa ya wananchi yalifanyika siku hiyo huko Iraqi dhidi ya wavamizi. Katika maandamano hayo yaliyofanyika mjini Baghdad tarehe 13 Aprili 2003, Wairaqi waliodhulumiwa kwa miaka mingi, walikuwa wakipinga nara za "Allah Akbar, La ilaha illallah" na "hatuitaki Marekani wala Israel". Waandamanaji hao waliwatangazia walimwengu kwamba hawataki majeshi vamizi nchini humo na kwamba George Bush na Saddam Hussein ni pade mbili za safaru moja.

Askari vamizi wa Marekani nchini Iraq

Tarehe 24 Farvardin miaka 14 iliyopita watu kadhaa waliuawa shahidi katika shambulizi la kigaidi lililofanyika katika mji wa Shiraz nchini Iran. Shambulizi hilo lilifanyika kwa bomu lililokuwa limetegwa kwenye kituo cha kidini cha Husainiya ya Mashahiri na kuua watu kadhaa na kujeruhi wengine. Jinai hiyo ilifanywa na vibaraka wa mashirika ya ujasusi ya nchi za kigeni. Baadhi ya vibaraka hao walikamatwa baada ya mlipuko uliotokea katika mojawapo ya hoteli za Tehran na kuadhibiwa kifo baada ya kufikishwa mahakamani. 

 

Tags