Jumanne, tarehe 19 Aprili 2022
Leo ni Jumanne tarehe 17 Ramadhani mwaka 1443 Hijria sawa na tarehe 19 Aprili 2022.
Miaka 2055 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nadharia za wanahistoria, yaani tarehe 19 Aprili mwaka 33 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as), kulianzishwa maktaba ya kwanza ya umma duniani 'Public Library' huko Roma ambayo kila mwenye elimu alikuwa na haki ya kuingia humo na kusoma vitabu alivyotaka. Kabla ya Waroma, Wasumeri, Waashuri, Wababeli na Wairani walikuwa na maktaba zao ingawa maktaba hizo hazikuwa zikitumika na watu wote, huku maktaba ya Waashuri ikiwa ndio maarufu zaidi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nchi ya kwanza ambayo ilianzisha asasi za uandishi na tarjama za vitabu duniani, ilikuwa ni Iran, ambapo karne 15 zilizopita zilikuwa zikifanya kazi hizo katika utawala wa Khosrow Anushirvan.

Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Isra inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka msikiti wa mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima za wanadamu katika ulimwengu wa Akhera.Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Tarehe 17 Ramadhani miaka 1441 iliyopita, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita yaani 19 Aprili mwaka 1882, alifariki dunia mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza Charles Darwin. Alizaliwa Februari 12 1809 nchini Uingereza. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu manma ya kudhihiri viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu na baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa. Fikra za Darwin zinapingana na mafundisho ya dini za mbinguni kuhusu namna ya kuumbwa mwanadamu lakini zimetumiwa kama msingi wa mifumo ya kiilhadi (isiyoamini uwepo wa Mwenyezi Mungu) kama ule wa Umaxi. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na alizikwa pembizoni mwa Isaac Newton katika kanisa la Westminster Abbey mjini London.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita yaani tarehe 19 Aprili 1995, kulitokea mlipuko mkubwa ulisababisha mauaji katika mji wa Oklahoma City nchini Marekani. Katika siku hiyo Timothy McVeigh alilipua bomu mbele ya jengo la Federali la mji wa Oklahoma City ambalo liliua watu 168. Mauaji hayo yalitambuliwa kuwa tukio kubwa zaidi la kigaidi katika historia ya Marekani kabla ya kutokea mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001. McVeigh alisema kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni upinzani wake dhidi ya serikali ya federali ya Marekani na kulipiza kisasi tukio la kuchomwa moto makao ya kundi la Davidian katika mji wa Waco mwaka 1993 lililopelekea kuuawa wafuasi 76 wa kundi hilo. Hujuma hiyo dhidi ya jengo la Federali ni tukio ambalo liliwaingiza woga na wahka Wamarekani na kubaini kuwa jamii ya nchi hiyo inakabiliwa na tishio kubwa la ugaidi wa ndani ya nchi.
Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Kadinali Joseph Ratzinger alikabidhiwa uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kufariki dunia Papa John Paul wa Pili na kuchagua jina la Papa Benedict wa 16. Ratzinger alizaliwa mwaka 1927 nchini Ujerumani na alipanda daraja na kuwa askofu mwaka 1977 na hatimaye kufikia daraja ya ukadinali. Papa Benedict wa 16 alikabiliwa na matatizo mbalimbali akiwa kiongozi wa kanisa hilo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa masuala ya kiroho katika nchi za Magharibi, ufisadi na utovu wa maadili pamoja na vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa na maaskofu na makasisi dhidi ya watoto wadogo. Papa Benedict wa 16 alilazimika kuachia uongozi wa Kanisa Katoliki Februari mwaka 2013 baada ya kuzongwa na kashfa nyingi za viongozi wa ngazi za juu ndani ya kanisa hilo.