Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (41)
Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.
Vipindi vyetu viwili vilivyotangulia vilitupia jicho historia na maisha ya Muhammad Baqir Majlisi mashuhuri kwa jina la Allama Majlisi. Tulieleza kuwa, Allama Majlisi alikuwa mmoja wa Maulamaa wa Kishia waliokuwa na taathira chanya na muhimu mno katika harakati za kisiasa na kijamii katika kipindi cha utawala wa Ukoo wa Safavi. Nafasi na daraja ya kielimu aliyokuwa nayo Allama Majlisi mbele ya matabaka mbalimbali ya watu katika jamii ilimfanya mtawala Shah Suleiman Safavi ampatie cheo cha Sheikh al-Islam. Hiyo ilikuwa mwaka 1098.
Sheikh al-Islam kilikuwa cheo cha juu kabisa cha kidini ambapo mwenye cheo hicho alikuwa amepatiwa wadhifa na utawala wa kusimamia masuala ya kisheria, kutoa hukumu yaani kama Kadhi Mkuu, kuwachagua na kuwauzulu makadhi, kusimamia masuala ya mayatima, kupokea na kutumia Khumsi na Zaka kwa ajili ya masuala yanayohusu jamii ya Waislamu na masuala mengine muhimu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 41 ya mfululizo huu kitaendelea kumzungumzia Allama Majlisi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Allama Majlisi ameandika vitabu vingi, lakini kitabu cha Bihar al-Anwar ambacho jina lake kamili ni Bihar al-Anwar, Al-Jamiatu Lidurari Akhbari al-Aimati al-At'har ndicho mashuhuri na muhimu zaidi miongoni mwa vitabu vyake. Kitabu hiki ni Dairatul Maarif yaani Ensaiklopidia kubwa ya hadithi za Waislamu wa madhehebu ya Shia ambayo imekusanya humo masuala yote ya kidini, kihistoria, fikihi, itikadi, Tafsiri ya Qur'ani na kadhalika.
Kitabu hiki kina zaidi ya hadithi 85,000 zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Ahlul-Baiti wake watoharifu (as). Ilimchukua Allama Majlisi miaka zaidi ya 30 kuandika kitabu hiki. Kundi la wanafunzi wa Allama Majlisi wakiwa chini ya usimamizi wake walikuwa na nafasi muhimu ya kuandika na kupatikana kitabu hiki.
Katika utangulizi wa kitabu hiki cha Bihar al-Anwar, Allama Majlisi amebainisha kipindi chake cha masomo na hatua pamoja na marhala zake za kielimu bila kusahau njia na mwenendo wake wa kimaanawi na kiroho. Aidha amebainisha sababu ya yeye kuegeme upande wa elimu na taaluma ya hadithi. Allama Majlisi alikuwa akiamini kwamba, Qur'ani na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as) ndio vyanzo muhimu zaidi vya kupokea na kuchota maarifa ya dini na kwamba, elimu hizo ziko juu ya elimu nyingine za Kiislamu.

Pamoja na hayo, msomi huyo hakuwa akipinga na kukataa nafasi na itibari ya akili bali alikuwa akiamini kwamba, kufahamu Misingi ya Dini kunafungamana na maarifa ya kiakili na katika baadhi ya mambo alikuwa akitumia hoja ya akili kuchambua na kufasiri baadhi ya hadithi.
Katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar, Allama Majlisi amezipanga hadithi kwa namna ya kimantiki na kulingana na maudhui ili wasomaji na wahakiki waweze kunufaika zaidi na kwa muda mfupi. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa katika majimui adhimu ya Bihar al-Anwar kuakisi maudhui na masuala yote ya kidini na kukusanya hadithi zinazohusiana na maudhui hizo. Kitabu hiki kinaanza na maudhui ya akili na ujinga na kisha kuendelea kwa kuzungumzia masuala yanayohusiana na kumtambua Mwenyezi Mungu, Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu), uadilifu wa Allah na historia ya Mitume (as).
Moja ya sifa muhimu za kitabu cha Bihar al-Anwar ni kwamba, katika kila mlango wa kitabu hiki, Allama Majlisi ameanza kwa majimui kubwa ya Aya za Qur'ani zinazonasibiana na maudhui husika. Baadhi ya wasomi na wanazuoni wanasema kuwa, katika kitabu cha Bihar al-Anwar kuna hadithi dhaifu na zisizo na itibari na kutokuweko maelezo ya kutosha ya Allama Majlisi na kwamba, hayo ni baadhi ya mambo yanayokifanya kitabu hiki kuwa dhaifu.

Katika kujibu ukosoaji huu inapasa kuzingatia kwamba, moja ya malengo ya Allama Majlisi katika kuandika na kualifu kitabu cha Bihar al-Anwar yalikuwa ni kukusanya hadithi ili kuzuia zisipotee ili kwa njia hiyo aweze kukifikishia kizazi kijacho cha Shia turathi na dafina hii, huku lengo la pili likiwa ni kufafanua, kubainisha na kufanya uchunguzi wa hadithi. Allama Majlisi alikuwa akitambuua kwamba, umri ni wenye kupita haraka na hivyo hataweza kupata fursa ya kuzichunguza na kuzifanyia utafiti hadithi zote. Ni kwa msingi huo ndio maana akaamua kuchukua hatua ya awali ya kwanza na ya kimsingi, ambayo ni kukusanya hadithi na afanye kile atakachojaaliwa katika kubainisha na kutoa ufafanuzi jumla wa hadithi hizo na kisha kuviachia vizazi vijavyo kazi ya uhakiki na ufafanuzi zaidi wa hadithi hizo.
Kundi jingine la wakosoaji wa kitabu cha Bihar al-Anwar linasema kuwa, kukaririwa hadithi ni moja ya nukta dhaifu za kitabu hiki. Hata hivyo kwa kutupia jicho maelezo na ibara za Allama Majlisi inafahamika kwamba, mwanazuoni huyu alikuwa akifahamu hali hiyo ya kukariri lakini hilo lilitokana na sababu mbalimbali likiwemo suala la hadithi moja kujumuisha maudhui mbalimbali ambapo kila maudhui inapaswa kuwa katika mlango wake na kujadiliwa.
Allama Majlisi aliishi umri uliokuwa na baraka kubwa. Katika umri wake wa miaka 73, Allama Majlisi aliandika vitabu zaidi ya 100 kwa lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku kitabu cha Bihar al-Anwar kikichapishwa kikiwa na mijalada 110 Vitabu vingine vya Allama Majlisi ni Hayatul-Qulub kuhusiana na historia ya Mitume (as), Jalaul-Uyun kuhusiana na maisha ya Maimamu Maasumina (as), Hilyatul-Mutaqin kuhusiana na adabu na ada maisha na Haqqul Yaqin kinachohusiana na masuala ya kiitikadi.

Wapenzi wasikilizaji katika vipindi vyetu viwili vilivyopita na hiki cha leo tumezungumzia maisha ya Allama Majlisi, msomi na mwanazuoni mahiri na mtajika katika Ulimwengu wa Kiislamu hususan Ulimwengu wa Kishia. Kile tulichowafikisha kukizungumzia katika sehemu hizi tatuu ni sehemu ndogo mno ya maisha ya mwanazuoni huyu ambaye kila lahadha na saa ya maisha yake ilitawaliwa na mafunzo na ibra pamoja na mazingatio ambayo inaweza kuwa mlango miongoni mwa milango ya elimu kwa watafutao elimu na wale wenye lengo la kunufaika na bahari ya kina kirefu ya elimu ya wasomi na Maulamaa kama Allama Majlisi.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.